1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi Sudan lafuta makubaliano ya mpito na kuitisha uchaguzi

Iddi Ssessanga
4 Juni 2019

Jeshi la Sudan limetangaza kufuta makubaliano ya kugawana madaraka lililokuwa limeafikiana na viongozi wa maandamano, na limeamua kuandaa uchaguzi katika kipindi cha miezi tisa, baada ya ukandamizaji wa kumuaga damu.

https://p.dw.com/p/3Jmns
Sudan Militärrat Abdel Fattah al Burhan
Mkuu wa Baraza la Kijeshi la Sudan Jenerali Abdel Fattah al-Burhan.Picha: picture-alliance/AA

Uamuzi huo umetangazwa siku moja baada ya jeshi kuwasambaratisha waandamanaji waliopiga kambi nje ya makao makuu yake kwa wiki kadhaa, na kusababisha mauaji ya watu zaidi ya 30.

Baraza la kijeshi la mpito lilimuondoa rais Omar al-Bashir mwezi Aprili baada ya miezi kadhaa ya maandamano dhidi ya utawala wake wa miaka 30 na lilikubali kuwepo kipindi cha mpito cha miaka mitatu ambamo lingekabidhi madaraka kwa uongozi wa kiraia.

Lakini Mkuu wa majeshi Jenerali Abdel-Fattah al-Burhan, ametangaza mapema leo kupitia televisheni, kuwa mpango huo umewekwa kando na uchaguzi utafanyika chini ya usimamizi wa kikanda na kimataifa.

"Baraza la Kijeshi limeamua juu ya yafuatayo: Kufuta yaliyokuwa yameafikiwa na kusimamisha majadiliano na muungano wa uhuru na mabadiliko, na kuitisha uchaguzi mkuu katika kipindi kisichozidi miezi tisa," alisema Jenerali al-Burhan.

Sudan Proteste in Khartum
Waandamanaji wakiimba nyimbo mitaani wakitaka jeshi likabidhi madaraka kwa raia mjini Khartoum, Juni 3, 2019.Picha: Reuters

Jumuiya ya kimataifa yalaani

Waandamanaji kadhaa wameuawa na mamia wengine walijeruhiwa siku ya Jumatatu, katika ukandamizaji wa umwagaji damu nje ya makao makuu ya jeshi mjini Khartoum, ambao umelaaniwa vikali na jamii ya kimataifa.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alikosoa matumizi ya nguvu ya kupitiliza dhidi ya waandamanaji na kutoa wito wa uchunguzi huru.

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lilipanga kukutana kwa faragha Jumanne kuijadili Sudan, baada ya Uingereza na Ujerumani kuomba mkutano huo, wamesema wanadiplomasia.

Kamati ya Madaktari wa Sudan, ambayo iko karibu na waandamanaji, ilisema idadi ya waliouawa iliongezeka na kuzidi 30, huku mamia wakijeruhiwa.

Chama cha wataalamu wa Sudan, ambacho kiliongoza maandamano ya nchi nzima yalioanza mnamo mwezi Desemba, kimewatolewa mwito Wasudan kushiriki katika uasi kamili wa kiraia ili kuupindua utawala wa kijeshi.

Sudan Soldaten in Khartum
Wanajeshi walitumwa na kusambaratisha maandamano yaliokita kambi nje ya makao ya jeshi mjini Khartoum, ambamo watu zaidi ya 30 waliuawa, Juni 3, 2019.Picha: Getty Images/AFP/M. El-Shahed

Pia kiliwataka raia kujitokeza na kushiriki swala ya Eidul Fitri, inayoashiria kumalizika kwa mwezi Mtukufu wa Ramadhani, kuwaombea mashahidi na kisha kuandamana kwa amani. Shirika la habari la Sudan SUNA limesema tarehe rasmi ya swala ya Eid ni Jumatano.

Wito wa kuwajibishwa wahusika

Mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa Afrika Moussa Faki, ametaka uchunguzi wa haraka na wa wazi ufanyike ili kuwawajibisha wote waliohusika katika ukandamizaji huo.

Shirika la kutetea haki la Amnesty International, limeitaka jamii ya kimataifa kuzingatia aina zote za shinikizo la amani, ikiwemo vikwanzo makhsusi dhidi ya maafisa wa baraza la mpito la kijeshi waliohusika na mashambulizi ya vurugu dhidi ya waandamanaji.

Muungano wa Uhuru na Mabadiliko ulitangaza mwisho wa mawasiliano yoyote ya kisiasa na majadiliano na  Baraza la kijeshi kufuatia vifo vya waandamanaji, licha ya Umoja wa Falme za Kiarabu na Misri kuzisihi pande mbili ziendelee kuzungumza.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe,rtre

Mhariri: Josephat Charo