1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi lazima jaribio la mapinduzi Sudan

Saumu Mwasimba
12 Julai 2019

Wanajeshi kadhaa wa ngazi ya juu wahusishwa na jaribio la mapinduzi dhidi ya baraza la kijeshi Sudan,kwa nia ya kuzuia utekelezaji wa makubaliano ya kisiasa yaliyofikiwa na yatakayosainiwa Jumamosi

https://p.dw.com/p/3LyWl
Sudan | Militärregierung PK Putschversuch  vereitelt
Picha: picture-alliance/AA

Maafisa takriban 16 wa kijeshi wamekamatwa kufuatia jaribio la mapinduzi ya kijeshi dhidi ya utawala wa muda unaoshikiliwa na baraza la kijeshi nchini Sudan. Luteni Jenerali Gamal Omar ambaye ni mjumbe wa baraza kuu la kijeshi linaloshikilia madaraka katika nchi hiyo amesema vikosi vya usalama vinaendelea hivi sasa kuwasaka maafisa wengine zaidi walioshiriki kwenye njama hiyo ya kutaka kufanya mapinduzi ya kijeshi jana alhamisi.

''Uhuru na kutangazwa mageuzi ni mambo yanayoleta matumaini na malengo ya watu wa Sudan kuondokana na utawala uliopita na kuangalia mbele katika kupatikana uthabiti  na usalama na kuwapatia Wasudan  walioanzisha vuguvugu takatifu la mapinduzi,maisha ya staha wanayostahili. Kutokana na hususan hali hii tunayoishi,vikosi vyetu vya usalama vimefanikiwa kuzima jaribio la mapinduzi yaliyoshindwa yaliyoandaliwa na kupangwa na kundi la maafisa wa juu jeshini,vikosi vya usalama na idara za kitaifa za usalama,kwa nia ya kufanya mapinduzi ya kijeshi  kutatiza utekelezaji wa makubaliano ya kisiasa  yaliyoiongoza nchi hii kuelekea kwenye mabadiliko ya kisiasa na kuyafikia mahitaji ya wananchi wetu.''

Baraza la kijeshi limesema waliokamatwa katika  njama hiyo wanne miongoni mwao ni maafisa  wastaafu jeshini. Sakata hili limetokea katika wakati mbaya kabisa ambapo unasubiriwa mchakato wa kutia saini makubaliano ya kisiasa.

Sudan Khartoum - Demonstranten fordern Machtübergabe des Militär an die Bevölkerung
Picha: Reuters/Stringer

Wiki iliyopita jeshi na muungano wa wanaopigania demokrasia nchini humo walikubaliana kuhusu baraza huru la pamoja la kusimamia uongozi wa nchi hiyo kwa kipindi cha kiasi miaka mitatu wakati nchi hiyo ikiandaa uchaguzi.

Umoja wa Afrika kupitia mjumbe wake wa ngazi ya juu Mohammed el Hassan Labat umeshathibitisha kwamba mchakato huo wa kusainiwa makubaliano ya kisiasa utafanyika kesho Jumamosi, tangazo ambalo limetolewa saa chache  tu baada ya jeshi la Sudan kudai limezima jaribio la mapinduzi jana usiku.Kadhalika msuluhishi kutoka Ethiopia Mohamoud Dirir akitoa ufafanuzi zaidi juu ya makubaliano kwa kueleza kwamba

''Waraka wa kisiasa umeshakubalika kwa sauti moja kilichobakia ni tangazo litakalochanganua kipindi cha mpito au kipindi cha mpito kuelekea serikali ya kiraia.Hili litajadiliwa na kuzungumzwa na kutiwa saini wakati mmoja''

Sudan Krise Vermittlungsversuch Äthiopien Premierminister Abiy Ahmed
Picha: picture-alliance/AA/M. Hjaj

Makubaliano ya kisiasa yanayosubiri kusainiwa ni njia inayodhamiriwa kuuvunja hatimae mkwamo wa kisiasa ulioikumba nchi hii tangu alipoangushwa madarakani rais aliyeiongoza kwa mkono wa chuma Omar al Bashir mwezi Aprili.

Mwandishi: Saumu Mwasimba

Mhariri: Mohammed Khelef