Jeshi la Myanmar lapinga cheo kipya cha Su Kyi | Matukio ya Kisiasa | DW | 01.04.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Jeshi la Myanmar lapinga cheo kipya cha Su Kyi

Bunge la Myanmar limepitisha mswaada wa dharura unaotengenezea cheo maalum kwa kiongozi wa NLD, Aung San Suu Kyi, cheo ambacho kinampa madaraka ya juu kuliko hata rais, licha ya katiba kumzuiwa kuwa rais wa nchi hiyo.

Myanmar Vereidigung Regierung - Außenministerin Aung San Suu Kyi

Kiongozi wa NLD Aung Su Kyi na baadhi ya majenerali wa jeshi la nchi hiyo

Taifa hilo la kusini Mashariki mwa Asi, limekuwa likiendeshwa na jeshi kwa zaidi ya nusu karne hadi siku ya Jumatano wiki hii wakati Suu Kyi na chama chake kinachotetea demokrasia NLD kilipochukua rasmi madaraka.

Tangu awali, Suu Kyi ambaye pia ni mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel, alishaapa kuiendesha nchi hiyo licha ya katiba kumyima nafasi ya kuwa rais.

Hapo jana, chama chake cha NLD kilichukua hatua ya kushtukiza bungeni kwa kupendekeza mswada wa kumpa nafasi ya kuwa mshauri mkuu wa kitaifa.

Myanmar Htin Kyaw Staatspräsident mit Aung San Suu Kyi Parteivorsitzende

Rais Htlin Kyaw wa Mnyanmar na Su Kyi

Iwapo mswada huu utapitishwa, basi Suu Kyi aliye na miaka 70 atakuwa na mamlaka ya kuendesha serikali, kando na kupewa nafasi nne za uwaziri katika baraza jipya la mawaziri katika serikali hiyo mpya. Nafasi hizo ni pamoja na wizara ya mambo ya nje, elimu, nishati na katika ofisi ya rais.

Jeshi lasema hatua iliyochukuliwa na NLD ni kinyume cha katiba

Hata hivyo, katika dalili za kwanza za mvutano kati ya serikali hiyo mpya na jeshi lililo na ushawishi mkubwa kwenye taasisi za utawala, wabunge wa kijeshi wameiita hatua hiyo kuwa kinyume cha katiba, katika mjadala uliyofanyika bungeni. Mbunge Kanali Myint Swe ameelezea wasiwasi wake kuwa nafasi hiyo itamuweka Suu Kyi katika nafasi sawa na Rais Htin Kyaw, ambaye ni rafiki na mshauri wa karibu wa Suu Kyi.

Myanmar Vereidigung Regierung - neuer Präsident Htin Kyaw

Rais mpya wa Mnyanmar Htin Kyaw

Mbunge mwengine kutoka upande wa kijeshi Kanali Hla Win Aung, pia amepinga hatua hiyo huku akionya kuwa itauharibu mfumo wa madaraka kati ya bunge, baraza la mawaziri na mahakama. Katiba ya Myanmar inalipa jeshi asilimia 25 ya viti katika mabunge yote mawili pamoja na haki ya kutumia kura yake ya turufu kupinga mabadiliko yoyote ya kikatiba.

Aung Sang Suu Kyi hawezi kuwania nafasi ya urais nchini humo kutokana na kipengele cha katiba kinachowanyima nafasi hiyo wale walio na familia za kigeni. Watoto wawili wa Suu Kyi na mume wake ambaye sasa ni marehemu ni raia wa Uingereza.

Wakati huo huo, waangalizi wa mambo wameelezea wasiwasi wao juu ya namna serikali hiyo mpya iliyochaguliwa na wananchi itaweza kupambana na changamoto katika nchi hiyo iliyokuwa na utawala wa kijeshi kwa miaka mingi.

Wachambuzi hao wanasema hatua hii iliyochukuliwa na chama cha NLD huenda ikavuruga mpango mzima wa uwepo wa demokrasia nchini Myanmar.

Mwandishi: Amina Abubakar/AFP

Mhariri: Mohammed Khelef

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com