1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la DR Congo limewakamata wanamgambo 14 wa ADF

John Kanyunyu25 Oktoba 2021

Jeshi la Congo limetangaza kukamatwa kwa wapiganaji kumi na wanne katika eneo la Beni mashariki mwa Congo na miongoni mwao kuna mke wa naibu kiongozi wa kundi la kigaidi kutoka Uganda ADF. 

https://p.dw.com/p/429AU
Demokratische Republik Kongo | Unruhen in Beni
Picha: Alexis Huguet/AFP/Getty Images

Wakati huo huo, ADF wanaendelea na mashambulizi yao dhidi ya vijiji mbalimbali na kuwauwa watu. 

Akizungumza na wanahabari katika mji huu wa Beni, msemaji wa jeshi la serikali katika operesheni dhidi ya ADF Captain Anthony Mualushayi alisema, kuwa, jeshi limefanikiwa kuwashika wapiganaji wa ADF na kubwa katika yote ni kushikwa pia kwa mke wa Amigo, naibu kiongozi wa ADF.

"Tumewaonesha wapiganaji kumi na wanne magaidi,miongoni mwao mna raia wa nchi za kigeni sita. Waganda, Tanzania, Wacongo na pia Warundi. Wakati roho ya kiongozi huyo wa magaidi inaguswa kwa kuwashika watu wake, lazima watalipiza kisasi. Sisi tunaelewa na ndio maana tunawaomba wakaazi kulielewa pia hilo. Sio jambo jepesi kuona mke anafungwa pamoja na wanawe wawili na yeye kama gaidi atafanya juu chini ili kulipiza kisasi. Tumesuka mikakati ili kuzuia mashambulizi ya adui dhidi ya raia, " amesema Anthony Mualushayi.

Kukamatwa kwa wapiganaji hao kunatokea, wakati ADF wamezidisha mashambulizi yao katika vijiji mbalimbali vya mikoa ya Kivu ya Kaskazini pamoja na Ituri. 

Katika mkoa wa Kivu ya Kaskazini, katika mji mdogo wa Bulongo, ADF waliwauwa watu zaidi ya thelathini mwishoni mwa wiki iliyopita. 

Shambulizi lililowapelekea wakaazi wengi kuuhama mji huo, ni lile la Jumamosi, ambako watu saba waliuawa na ADF, kama wanavyotueleza wakaazi hawa wa Bulongo ambao wamelazimika kutoroka. 

Wanamgambo wa ADF wamekuwa wakifanya mashambulizi ya mara kwa mara na kuwaua watu katika mikoa ya Beni na Ituri inayokumbwa na machafuko
Wanamgambo wa ADF wamekuwa wakifanya mashambulizi ya mara kwa mara na kuwaua watu katika mikoa ya Beni na Ituri inayokumbwa na machafukoPicha: Alexis Huguet/Getty Images/AFP

Mbali na mauwaji ya Bulongo usiku wa kuamkia jana Jumapili, ADF waliwauwa watu wengine katika kijiji cha Kapalata, kilomita thelathini hivi Kaskazini mwa mji wa Beni.

Nao wakaazi wa kijiji cha Ngadula, kilomita kumi hivi magharibi mwa Oicha mji mkuu wa wilaya ya Beni, wanasemekana kuwa wanayatoroka mashamba yao, kufuatia uwepo wa ADF katika viunga vya kijiji hicho.

Haya yote yanatokea, wakati naibu katibu mkuu wa Umoja wa mataifa anayehusika na operesheni za kusimamia amani Jean-Pierre La Croix akiwa ziarani katika nchi hii. 

Mwishoni mwa wiki iliyopita, La Croix alizuru mji wa Beni, ambako alikutana kwa mazungumzo na viongozi wa jeshi katika operesheni dhidi ya ADF, pamoja na wajumbe wa mashirika ya kiraia.

Wajumbe wa mashirika ya kiraia walimuomba La Croix kufanya juu chini ili Monusco kupitia kikosi chake maalumu cha kuingilia kati kufanya operesheni za pamoja na jeshi la Congo kwani, ikiwa jeshi la Congo halitofanikiwa kuwatokomeza ADF wanaowauwa watu hapa, Umoja wa mataifa nao utalaumiwa kwa kufeli katika majukumu yake.