1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Japan na Korea ya Kusini zapania kumaliza mivutano

Oumilkheir Hamidou
13 Oktoba 2019

Waziri mkuu wa Korea ya Kusini ataitembelea Japan wiki ijayo,kwa mara ya kwanza tangu Japan ilipoiwekea vizuwizi vya biashara nchi hiyo na kupalilia mizozo ya kibiashara na kidiplomasia kati ya nchi hizi mbili.

https://p.dw.com/p/3RCxp
Japan - Kaiser Naruhito wird neuer Kaiser Japans
Picha: Reuters/Kyodo

Kwa mujibu wa ofisi ya waziri mkuu, Lee Nak-yon aliyepanga kuitembelea Japan kati ya October 22 hadi 24, atahudhuria pia sherehe za kuvikwa taji , mfalme Naruhito. Anatarajiwa kushiriki katika hafla itakayoandaliwa na waziri mkuu Shinzo Abe na kufanya mazungumzo baadaye pamoja nae, mazungumzo yatakayokuwa ya ngazi ya juu kabisa kuwahi kufanyika tangu mvutano ulipozuka mwaka jana kuhusu madai kwamba Japan iliwalazimisha  wa Korea ya Kusini wafanye kazi za sulubu wakati wa vita vikuu vya pili vya dunia.

"Tunataraji ziara hii itasaidia, kwakuwa pande hizi mbili zinatambua umuhimu wa kuendeleza mazungumzo ili kuimarisha uhusiano", afisa  mmoja wa serikali ambae hakutaka jina lake lijulikane amesema.

Uhusiano kati ya majirani hao wawili umeharibika vibaya sana tangu uliporejeshwa kuwa wa kawaida mwaka 1965 baada ya korti kuu ya Korea ya Kusini kuamuru mwaka jana makampuni mawili ya Japan yawalipe fidia wafanyakazi wa enzi za vita.

Uhusiano wa kiuchumi kati ya Japan na Korea ya Kusini umedhoofika
Uhusiano wa kiuchumi kati ya Japan na Korea ya Kusini umedhoofikaPicha: Getty Images/AFP/Jung Yeon-Je

Urafiki wa viongozi hao wawili huenda ukasaiodia kumaliza uhasama

Japan inasema mzozo huo umeshatatuliwa kwa kutiwa saini mkataba wa mwaka 1965 uliourejesha katika hali ya kawaida uhusiano kati ya nchi hizo mbili.

Mvutano huo umechukua sura nyengine na kuathiri pia masuala ya biashara na usalama huku Japan ikiwekea vizuwizi biashara yake kuelekea Korea ya Kusini huku Korea ya Kusini  nayo ikisitisha mkataba wa ushirikiano kati ya idara za upelelezi za nchi hizo mbili.

Waziri mkuu  Shinzo Abe na kiongozi mwenzake wa Korea ya Kusini, Lee Nak-yon, mwandishi habari wa zamani aliyewahi kuwa ripota nchini Japan, wameanzisha uhusiano madhubuti tangu walipoanza kujishuhulisha na siasa. Wamekutana kwa mara ya mwisho katika kongamano la kimataifa nchini Urusi mwezi septemba mwaka 2018.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters

Mhariri. Tatu Karema