1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yaendelea kuipiga Gaza licha ya ukosoaji wa Marekani

13 Desemba 2023

Israel imeendeleza mashambulizi yake ya angani na ardhini dhidi ya Ukanda wa Gaza, Jumatano, na kusababisha gadhabu za kimataifa na ukosoaji usio wa kawaida kutoka Marekani, kuhusiana na kuuwa maelfu ya raia.

https://p.dw.com/p/4a7m8
Ukanda wa Gaza | Moshi ukifuka juu ya mji wa Khan Younis.
Picha iliyochukuliwa kutokea Rafah ikionesha moshi ukifuka juu ya mji wa Khan Younis kusini mwa Gaza wakati wa mashambulizi ya Israel mapema Desemba 12, 2023.Picha: SAID KHATIB/AFP/Getty Images

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipiga kura kwa wingi hapo jana kutaka usitishaji mapigano kwa ajili ya masuala ya kibinadumu, katika azimio lisilo na nguvu ya kisheria, lakini lenye kutuma ujumbe madhubuti kuhusu hisia za ulimwengu juu ya vita hivyo.

Saa chache tu kabla ya kura hiyo,Rais wa Marekani Joe Biden alionya kuwa Israel ilikuwa inapoteza uungwaji mkono wa kimataifa kutokana na "mashambulizi yake yanawaua raia kwa wingi."

Vita vya Israel na Hamas katika ukanda unaotawaliwa na Hamas wa Gaza, vimesababisha vifo vya watu wasiopungua 18,608, kwa mujibu wa wizara ya afya ya Gaza, ambayo takwimu zake hazitofautishi kati ya vifo vya raia na wapiganaji.

Soma pia:Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lataka usitishaji mapigano mara moja Gaza 

Msemaji wa wizara hiyo Ashraf al-Qudra, amesema watu 50,594 wamejeruhiwa katika mzozo huo.

Israel inasema wanajeshi wake 113 wameuawa tangu ilipoanzisha mashambulizi ya ardhini, katika kampeni ya kisasi baada ya Hamas kufanya uvamizi wa kushtukiza kusini mwa Israel na kuuwa watu 1,200 na kuwachukuwa mateka wengine wapatao 240.

Maombolezo| Mpalestina akilia mbele ya maiti za wenzake zilizofungwa kwenye mifuko.
Wizara ya afya ya Gaza imesema Wapalestina zaidi ya 18,600 wameuawa tangu Oktoba 7, 2023, huku zaidi ya 50,000 wakijeruhiwa. Picha: DW

Huku hospitali zikiwa zimefurika, barabara zikiwa zimeharibiwa na ugavi wa mahitaji muhimu ukipungua pakubwa, watoto wanaozaliwa Gaza wanakabiliwa na mazingira magumu kuweza kuishi. Wakati huo huo, uchunguzi wa maoni ya Wapalestina umeonyesha kuongezeka kwa uungwaji mkono wa Hamas, huku karibu asilimia 90 wakitaka Rais Mahmoud Abbas anaeungwa mkono na Marekani ajiuzulu.

Wapalestina wauawa katika uvamizi wa Israel wa kambi ya wakimbizi Ukingo wa Magharibi


Takriban Wapalestina saba waliuawa na dazeni kadhaa walikamatwa wakati wa uvamizi wa Israeli wa siku mbili kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi.

Jeshi la Israel lilisema Jumatano kwamba wanajeshi wanaohudumu katika kambi ya wakimbizi ya Jenin walikamata silaha, risasi na vilipuzi, na kufichua mashimo ya chini ya ardhi, vituo vya uchunguzi na maabara sita za milipuko.

Wizara ya Afya ya Palestina imesema Wapalestina saba waliuawa huko Jenin Jumanne.

Kambi hiyo ya wakimbizi ya mijini yenye msongamano kwa muda mrefu imekuwa ngome ya wanamgambo wa Kipalestina. Vikosi vya Israel vimekuwa vikifanya mashambulizi ya mara kwa mara katika kipindi cha miaka miwili iliyopita ambayo mara nyingi yamezusha mapigano ya risasi na wapiganaji wa Kipalestina.

Soma pia:Israel yakanusha kutaka kuwahamishia Misri wakaazi wa Gaza 

Israel iliuteka Ukingo wa Magharibi, Jerusalem mashariki na Gaza katika vita vya Mashariki ya Kati vya 1967, na Wapalestina wanataka maeneo yote matatu ili kuunda taifa lao la baadaye.

Zaidi ya Wapalestina 270 wameuawa katika Ukingo wa Magharibi tangu kuanza kwa vita vya Israel na Hamas, kulingana na Wizara ya Afya.

Ukanda wa Gaza | Mashambulizi ya Israel katika mji wa Gaza wa Rafah
Asilimia kubwa ya miundombinu na majengo ya Gaza vimeharibiwa katika mashambulizi ya Israel.Picha: Hatem Ali/AP/picture alliance

Askari 9 wa Israel wauawa katika uvamizi mjini Gaza

Vyombo vya habari nchini Israel vinasema wanajeshi wasiopungua tisa waliuawa katika shambulizi la kuvuzia mjini Gaza, wakiwemo Kanali Itzhak Ben Basat, afisa wa juu zaidi kuuawa tangu kuanza kwa operesheni ya ardhini mwishoni mwa mwezi Oktoba, na Luteni Kanali Tomer Grinberg, kamanda wa Bataliani ya 13 ya Brigedi ya Golani.

Redio ya jeshi ilisema wanajeshi hao walikuwa wanafanya msako kwenye majengo walipoteza mawasiliano na wanajeshi wanne walioshambuliwa, na kuzusha hofu ya uwezekano wa kutekwa na wapiganaji wa Hamas.

Baada ya wanajeshi wengine kuanzisha operesheni ya uokozi, walizingirwa na mashambulizi makali na viripuzi. Jeshi lilithibitisha jumla ya wanajeshi 10 kuuawa Gaza siku ya Jumanne, lakini halikujibu masuali kuhusiana na mazingira.

Soma pia: Vita vya Israel-Hamas: Guterres atumia ibara ya 99 ya UN

Hamas ilisema shambulizi hilo lilionyesha kuwa mashambulizi ya Israel yamefeli. Marekani, Umoja wa Ulaya, Ujerumani na mataifa kadhaa mengine yanairodhesha Hamas kama kundi la kigaidi.

Papa Francis arejelea wito wa amani wa Gaza

Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis, amerudia wito wake wa kuwepo na usitishwaji vita kwa misingi ya kiutu, na kwa mateka wote waliochukuliwa na Hamas wakati wanamgambo wake walipoishambulia Israel mnamo Oktoba 7 kuachiwa.

Marekani| Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limepiga kura kwa wingi kutaka usitishaji mara moja wa vita wa kiutu, katika hatua iliyodhihirisha hisia za kimataifa kuhusu vita hivyo.Picha: ANGELA WEISS/AFP

"Pande zote mbili zinazohusika ziwe na ujasiri wa kuanza mazungumzo tena, na ninaomba kila mtu achukue kazi ya haraka ya kupata misaada ya kibinadamu kwa wakazi wa Gaza. Wako mwisho wa kamba yao na wanaihitaji sana," alisema.

"Achieni huru mateka wote mara moja walioona matumaini katika usitishaji mapigano siku chache zilizopita, naomba mateso haya makubwa kwa Waisrael na Wapalestina yakome. Tafadhali semeni hapana kwa silaha na ndiyo kwa amani."

Francis ametaka kuendeleza msimamo wa jadi wa Vatican wa kutoingilia katika mizozo, lakini amewagadhabisha Waisrael hasa kwa kuvitaja vita kwamba vinaelekea kuwa "ugaidi" bila kuilaani wazi Hamas kwa shambulizi lake la awali.

Makombora mawili kutoka eneo la Wahouthi yaikosa meli karibu na Yemeni

Makombora mawili ya masafa yaliyofyatuliwa kutoka eneo linalodhibitiwa na waasi wa Kihouthi nchini Yemen yaliikosa meli ya kibishara karibu na ujia wa bahari wa Bab al-Mandeb siku ya Jumatano, wamesema maamfisa wa Marekani.

Soma pia:Gaza ni 'jehanamu ya dunia' - Lazzarini 

Meli ya kivita ya Marekani pia ilidungua droni inayoshukiwa kutumwa na Wahouthi, ikiruka kuelekea upande wake wakati wa tukio hilo, alisema afisa, ambaye alizungumza kwa sharti la kutotajwa jina kujadilia masuala ya intelijensia. Hakuna aliedhurika katika shambulizi hilo, alisema afisa huyo.

Sikiliza pia: 

Azimio la Baraza Kuu la UM ina maana gani kwa mzozo wa Gaza?

Meli iliyolengwa, ya mafuta na kemikali kwa jina la Ardmore Encounter, ikipeperusha bendera ya visiwa vya Marshall, ilikuwa inasafiri kaskazini kuelekea ujia wa bahari wa Suez katika bahari ya Shamu, kwa mujibu wa picha za satelaiti zilizochambuliwa na shirika la habari la Associated Press.

Meli hiyo ilikuwa inatokea India na ilikuwa na wafanyakazi wa usalama waliojihami kwa silaha, kwa mujibu wa data zilizotolewa na meli hiyo. Wahouthi hawakukiri mara moja kuhusu shambulizi hilo.

Chanzo: Mashirika