Ingolstadt yatinga daraja la kwanza Bundesliga
18 Mei 2015Kwa FC Ingolstadt ni ndoto iliyotimia. Timu hiyo ya daraja la pili imepiga hatua na kuingia katika ligi daraja la kwanza nchini Ujerumani Bundesliga kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya RB Leipzig na kujihakikishia ubingwa wa ligi daraja la pili.
Mashabiki walimiminika uwanjani na kushangiria pamoja na kocha wao aliyeleta mafanikio Ralph Hasenhüttl.
Timu nyingine zinabidi kusubiri hadi wiki ijayo kufahamu iwapo zimefanikiwa kuingia daraja la kwanza . Darmstadt 98 imeshindwa kujihakikishia kuingia daraja la kwanza baada ya kupigwa mweleka na SpVgg Greuther Fürth kwa bao 1-0. Wapinzani wao FC Kaiserslautern bado ina nafasi ya kupanda daraja.
Borussia Monchengladbach itacheza msimu ujao katika Champions League awamu ya makundi kwa mara ya kwanza baada ya kuishinda Werder Bremen kwa mabao 2-0 na kujiakikishia nafasi ya tatu juu ya msimamo wa ligi ikiwa umebakia mchezo mmoja.
Schalke 04 imeokoa nafasi yake ya kucheza katika Ligi ya Europa, Europa League katika msimu wa kukatisha tamaa kabisa nyumbani kwa ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Parderborn , baada ya mlinzi wa timu hiyo Uwe uenemeier kujifunga mwenyewe.
VFB Stuttgart imefufua matumaini ya kubakia katika daraja la kwanza kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Hamburg SV ambayo nayo inawania kujitoa kutoka katika hatari ya kushuka daraja, ambapo sasa imeteremka tena hadi nafasi ya 17. Kocha wa Stuttgart Huub Stevens baada ya ushindi huo muhimu alikuwa na haya ya kusema.
"Naweza tu kutoa sifa nyingi kwa timu, kwamba vijana baada ya kuwa nyuma kwa bao moja waliweza kutuliza vichwa vyao, na kufanikiwa kupata bao la kusawazisha na baada ya hapo wakapata bao la pili. Bado tuna mchezo mmoja muhimu mbele yetu. Na baada ya hapo itakuwa imeamuliwa , iwapo tumefanikiwa ama la."
Hamburg inaweza kushuhudia rekodi yake kama timu ambayo haijawahi kushuka daraja katika Bundesliga tangu kuundwa kwa ligi hiyo mwaka 1963 ikichafuliwa na kufika mwisho wiki ijayo ambapo inapambana dhidi ya Schalke 04. Kocha Bruno Labbadia wa Hamburg amesema amefadhaika sana.
"Nimesikitika sana , kwamba mchezo huu umetuponyoka kutoka mkononi mwetu, mchezo ambao tulikuwa tayari tumeudhibiti, hususan baada ya kuongoza kwa bao moja. Lakini baada ya hapo tulikuwa na hali fulani , ambayo haikuwa nzuri kwetu. Na Stuttgart ilitumia vizuri hali hiyo."
Bayern Munich imeingia katika lawama kubwa, kwamba haijaonesha hali ya uwezo wake na kucheza chini ya kiwango na hali hiyo imeipa nafuu FC Freiburg ambayo ilifanikiwa kupata ushindi muhimu wa kuinyanyua kutoka nafasi ya chini na kuipa matumaini ya kubakia katika daraja la kwanza.
Huyu hapa kocha wa SC Freibug Christian Streich.
"Wakati tulikuwa tumeanguka , sasa tumesimama tena. Na sasa hatutaanza tu kujitayarisha kuruka. Tunapaswa kuchukua pointi kule Hannover, na tunapaswa kuonesha mchezo mzuri. Hii ina maana , sio zaidi na sio pungufu. Na ni hivyo tu unaweza kubakia katika daraja.
Nae kocha wa mabingwa Bayern Munich Pep Guardiola baada ya kipigo hicho cha nne mfululizo katika Bundesliga msimu huu amesema:
"Mchezo wa mwisho katika bundesliga baada ya ubingwa sio rahisi. Lakini ni sawa tu. Kuna mchezo mmoja zaidi dhidi ya Mainz na baada ya hapo likizo na baada ya hapo tutaangalia hali ya baadaye. Lakini naipongeza Freiburg kwa ushindi. Na ni matumaini yangu naweza kubakia mwaka ujao."
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / afpe 7 dpae
Mhariri: Iddi Ssessanga