Idadi ya watu kufikia bilioni 9.7 duniani
18 Juni 2019Idadi ya watu duniani inakuwa na wazee zaidi na ukuaji ni kwa kasi ndogo lakini bado inatarajiwa kuongezeka kutoka idadi ya sasa ya watu bilioni 7.7 hadi kufikia bilioni 9.7 ifikapo mwaka 2050. Idara ya Umoja wa mataifa ya masuala ya uchumi katika kitengo cha idadi ya watu imesema katika ripoti kwamba idadi ya watu inaweza kufikia kiwango chake cha juu cha karibu watu bilioni 11 kuelekea mwishoni mwa karne hii.
Lakini mkurugenzi wa idara ya idadi ya watu John Wilmoth ameonya kuwa kwasababu mwaka 2100 uko mbali kwa miongo mingi bado ,matokeo haya "hayana hakika" , na mwishoni kiwango cha juu kinaweza kuja mapema ama baadaye, katika kiwango cha juu ama cha juu cha jumla ya idadi ya watu."
Utabiri mpya wa idadi ya watu unaonesha kuwa nchi tisa zitahusika na zaidi ya nusu ya ukuaji unaotabiriwa wa idadi ya watu kati ya hivi sasa na mwaka 2050.
Nchi wachangiaji wa idadi ya watu
Nchi ambazo zitahusika na kuiongezea dunia idadi kubwa ya watu kuanzia ile ya juu hadi ya chini ni pamoja na India , Nigeria, Pakistan, Congo, Ethiopia, Tanzania, Indonesia, Misri na Marekani.
Katika eneo la Afrika kusini mwa jangwa la Sahara , idadi ya watu inakadiriwa kuongezeka maradufu ifikapo mwaka 2050, ripoti hiyo imesema.
Msaidizi wa katibu mkuu anayehusika na uchumi na masuala ya jamii Lu Zhenmin amesema katika taarifa, kwamba "Nyingi ya nchi zenye ukuaji mkubwa wa idadi ya watu ziko katika mataifa masikini, ambako ukuaji wa idadi ya watu unaongeza changamoto katika juhudi za kufuta ujinga," kuhimiza usawa wa kijinsia na kuwezesha hali bora ya huduma za afya na elimu.
Ripoti hiyo inathibitisha kuwa idadi ya wazee duniani inaongezeka kutokana na kupanda kwa kiwango cha matarajio ya kuishi na kupungua kwa viwango vya uzazi.