1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Idadi ya wasiokuwa na chakula yaongezeka

Saumu Mwasimba
11 Septemba 2018

Umoja wa Mataifa umedhihirisha kwamba idadi ya watu duniani wasiokuwa na chakula imeongezeka kwa kiwango kikubwa cha kutia wasiwasi.Watu milioni 821 wamekosa chakula 2017

https://p.dw.com/p/34fht
Malawi Schülerinnen und Schüler der Grundschule in Mkundi Region Dedza
Picha: imago/epd/S. Vogt

Umoja wa Mataifa unasema idadi ya watu wanaokabiliwa na njaa duniani inazidi kuongezeka na kurejea katika viwango vya kuanzioa muongo mmoja uliopita kufuatia mabadiliko ya tabia nchi.Katika ripoti ya mashirika makubwa ya Umoja wa Mataifa ya kila mwaka iliyotolewa leo, inaelezwa kwamba idadi ya wenye njaa wanaokabiliwa na ukosefu mkubwa wa chakula imeongezeka hadi kufikia watu milioni 821 katika mwaka 2017 kutoka watu milioni 804. Hali inatisha zaidi  Amerika Kusini na Afrika.

Mkuu wa shirika la mpango wa chakula duniani WFP David Beasley akizungumza katika mkutano na waandishi habari mjini Rome amesema kwamba ujumbe  uliotolewa leo kuhusu hali ya njaa duniani unapaswa kuuogopesha ulimwengu.Beasley amesema mabadiliko ya tabia nchi pamoja na migogoro ya kivita ni mambo yanayochochea kuongezeka kwa utapiamlo duniani kote.

Uganda Afrika Super Beans
Picha: picture-alliance/AP Photo/R. Muhumuza

Kwa mujibu wa ripoti hiyo  iliyopewa jina hali ya usalama wa chakula pamoja na virutubisho duniani,hali ya njaa imekuwa ikiongezeka katika kipindi cha miaka mitatzu  na kurejea katika hali ilivyokuwa muongo mmoja uliopita. Eneo la Mashariki mwa Afrika limetajwa katika ripoti hiyo ikieleza kwamba hususan mataifa yanayokabiliwa na migogoro kama Eritrea na Sudan Kusini ndiyo yaliyoathirika zaidi ambapo asilimia 31.4 ya wakaazi wake wanatajwa kuwa katika hali isiyokuwa ya lishe bora.Ripoti hii imechapishwa kwa juhudi za shirikiano wa mashirika ya UNICEF,WHO,FAO,IFAD sambamba na WFP.Mashirika hayo ambayo yote ni ya Umoja wa Mataifa yamegundua kwa mara ya kwanza juu ya kuongezeka kwa idadi ya wasiokuwa na chakula mwaka jana.

Migogoro,hali mbaya ya kiuchumi na majanga ya asili ni mambo yanayotajwa kusababisha hali hii mbaya ambapo mashirika hayo yameelezea wasiwasi wake kwamba Malengo ya maendeleo ya Umoja wa Mataifa  ya kufikia hatua ya kutokomeza njaa duniani kufikia 2030 yanaweza kuwa hatarini.Idadi ya majanga yanayotokana na mabadiliko ya tabia nchi ikiwemo ukame mkali,joto kali,mafuriko na vimbunga ni matukio yaliyoongezeka tangu mapema mwaka 1990.Hayo ni kwamujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa kuhusu njaa.Aidha ripoti hiyo imegundua kwamba watoto 151 milioni walioko chini ya umri wa miaka 5 ambao ni asilimia 22 ya jumla ya idadi ya watu duniani wameathirika ikiwa na maana kwamba muonekana wao katika ukuaji ni tafauti na umri walionao.

Kadhalika imefafanua ripoti hiyo kwamba watu wazima milioni 672 mmoja kati ya kila watu wanane kwenye idadi hiyo ana unene wa kupindukia idadi ambayo ni kubwa zaidi ikilinganishwa na mwaka 2014 ambapo ilikuwa ni watu milioni 600. Umoja wa mataifa pia unasema mwaka jana takriban watu milioni 124 katika nchi 51 wamekabiliwa na ongezeko la kupanda kiwango cha njaa kilichosababishwa na migogoro,pamoja na majanga ya kimazingira.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:Josephat Charo.