Idadi ya waliokufa kwa mafuriko Nepal yafikia 148
29 Septemba 2024Tangazo limetolewa huku timu ya uokoaji zikiwa zimeipata miili mingine kadhaa kwenye mabasi yaliofukiwa na maporomoko ya ardhi. Leo Jumapili maafisa nchini humo wamesema takriban watu 55 hawajulikani walipo.
Aidha msemaji wa jeshi la polisi Nepal Dan Bahadur Kark amesema, watu 101 wamejeruhiwa kwenye maafa hayo tangu siku ya Ijumaa na kuongeza kwamba familia zilizokumbwa na mkasa huo zimehamishiwa sehemu salama.
Kulingana na Kark takriban watu 3,661 wamehamishiwa maeneo salama, pamoja na kupatiwa mahitaji muhimu kutoka kwa serikali ikiwemo matibabu na chakula.
Kulingana na serikali zaidi ya nusu ya vifo vimetokea katika mji mkuu wa Kathmandu pamoja na wilaya jirani ambazo zilishuhudia mafuriko makubwa na maporomoko ya ardhi mabaya zaidi kushuhudiwa kwa miongo kadhaa.