1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Asili na mazingiraMarekani ya Kusini

Idadi ya waliofariki Venezuela yafikia watu 1,450

29 Juni 2026

Watu 1,450 wamefariki dunia na zaidi ya wengine 3,200 kujeruhiwa kutokana na matetemeko ya ardhi nchini venezuela huku ikikabiliwa na ukosoaji unaoongezeka kutoka kwa raia wake kuhusu mwitikio wa janga hilo.

https://p.dw.com/p/5GEf6
Venezuela La Guaira 2026 | Juhudi za uokoaji
Juhudi za kuwatafuta manusura wa matetemeko ya ardhi zaendelezwa nchini Venezuela, Juni 28, 2026Picha: Cem Tekkesinoglu/Anadolu/picture alliance

Maelfu ya waokoaji wa ndani na wa kimataifa wamekuwa wakijitahidi kuwaokoa manusura waliokwama chini ya vifusi vya majengo yalioporomoka, siku nne baada ya matetemeko mawili makubwa ya ardhi kulikumba jimbo la kaskazini la La Guaira.

Matumaini ya kuwapata  manusura yanaendelea kupungua kila saa inapopita.

Wataalamu wanaonya kuwa kipindi muhimu cha kuwapata manusura hupungua kwa kasi baada ya masaa 72, jambo linaloongeza hofu kwamba muda unazidi kuwatupa mkono wale ambao bado wamekwama chini ya vifusi.

Uokoaji kuendelezwa licha ya kupita kwa kipindi muhimu

Rais wa mpito wa Venezuela, Delcy Rodríguez, amesema licha ya kipindi hicho muhimu cha uokoaji kupita, juhudi za kuwatafuta manusura zitaendelea.

Amesema anaunda tume maalum ya kutathmini uharibifu wa nyumba ili kubaini kama ni salama kwa watu wanaolala nje kurejea makwao.

"Tunaunda kikosi kazi maalum kitakachoanzisha kambi za muda kwa watu waliopoteza makazi yao na kufanya mipango ya miradi itakayowezesha nyumba kujengwa ndani ya kipindi kifupi sana."

Rodríguez pia asema serikali yake itachunguza kiwango cha uharibifu wa miundombinu.

Maelfu ya watu waaminika bado kukwama chini ya vifusi

Spika wa bunge la nchi hiyo Jorge Rodríguez amesema inaaminika kuwa maelefu ya watu bado wamekwama chini ya vifusi.

India New-Delhi 2026 | Delcy Rodríguez akutana na Narendra Modi
Rais wa mpito wa Venezuela, Delcy Rodríguez akiwa ziarani nchini India kwa mkutano na waziri mkuu wa nchi hiyo Narendra Modi mjini New Delhi mnamo Juni 4, 2026Picha: Manish Swarup/AP Photo/picture alliance

Rodríguez amesema matetemeko hayo ya ardhi yenye ukubwa wa 7.2 na 7.5 kwenye kipimo cha ritcher yaliyotokea mfululizo siku ya Jumatano yalifuatiwa na mitetemeko mingine 430 midogo.

Umoja wa Mataifa nao umesema kuwa hadi watu milioni 6.8 kati ya wakazi karibu milioni 30 wa Venezuela huenda wameathirika na matetemeko hayo ya ardhi.

China kuongeza msaada kwa Venezuela

China imeelezea wasiwasi kuhusu matetemeko hayo ya ardhi na imeamua kuongeza msaada wa vifaa vya dharura vya thamani ya dola milioni 14.72 kwa  Venezuela  bila malipo. Haya yamesemwa leo na msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa nchi hiyo ​Guo Jiakun.

Jiakun amekiambia kikao cha kawaida cha waandishi wa habari kwamba bidhaa hizo zitapelekwa Venezuela haraka iwezekanavyo na kwamba iko tayari kutoa msaada zaidi.

Tathmini ya uharibifu uliosababishwa na matetemeko ya ardhi

Matetemeko hayo ya ardhi yamesababisha uharibifu mkubwa katika jimbo la pwani la La Guaira na katika mji mkuu, Caracas, ambapo ghorofa zote za majengo marefu ziliporomoka.

Kulingana na tathmini ya uharibifu ya hivi karibuni, zaidi ya majengo 2,500 ya makazi na miundombinu mingine yameporomokakabisa au yameharibika vibaya, ikiwa ni pamoja na takriban nyumba 780 na hospitali 38.