1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

HRW yalaani matumizi ya silaha nzito maeneo ya raia Sudan

Grace Kabogo
4 Mei 2023

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch limelaani vikali matumizi ya silaha za kivita katika maeneo yenye makaazi ya watu nchini Sudan.

https://p.dw.com/p/4Qv3K
Sudan Khartum Kämpfe
Picha: AFP

Mtaalamu wa masuala ya haki wa Human Rights Watch, Mohamed Osman amesema majeshi ya pande zinazohasimiana nchini Sudan yanatumia kiholela silaha zisizo sahihi katika maeneo ya mijini yenye watu wengi na hivyo kutojali maisha ya raia. Taarifa iliyotolewa Alhamisi na shirika hilo, imelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuongeza juhudi za kuhakikisha usalama wa raia na kuwawajibisha wanaohusika na mapigano hayo.

Wapiganaji wanaingia kwenye nyumba za watu

Shirika hilo limesema, watu walioshuhudia wameripoti kuwa makombora yaliwekwa na kurushwa katika maeneo ya karibu na majengo ya makaazi. Imeelezwa kuwa wapiganaji wa kikosi maalum cha wanamgambo wa RSF waliingia na kulala kwenye nyumba za jirani. Pia walitafuta makaazi nyuma ya nyumba kutokana na mashambulizi ya jeshi, hivyo kuyafanya majengo hayo kuwa yanayolengwa.

Wakati huo huo, Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi, UNHCR limesema dola milioni 445 zinahitajika kwa ajili ya kuwasaidia watu 860,000 ambao wanaweza wakawa wameikimbia Sudan ifikapo mwezi Oktoba. UNHCR imesema mapema leo kuwa iliwasilisha ombi lake kwa nchi wafadhili na kwamba fedha hizo zitapelekwa kuwasaidia Wasudan wanaokimbilia Chad, Sudan Kusini, Misri, Ethiopia na Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Sudan Flüchtlingswelle
Wakimbizi wa Sudan ambao wamevuka mpaka na kuingia ChadPicha: Gueipeur Denis Sassou/AFP

Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, zaidi ya watu 100,000 wameyakimbia makaazi yao tangu yalipozuka mapigano ya kugombania madaraka kati ya kiongozi wa kijeshi wa Sudan Abdel Fattah al-Burhan, na mkuu wa kikosi cha RSF, Mohamed Hamdan Daglo. Watu wengine 300,000 wamekuwa wakimbizi wa ndani ya Sudan.

Juhudi za kusitisha mapigano zaendelea kukwama

Tangazo hilo la Alhamisi limetolewa wakati ambapo milio ya risasi na miripuko imeshuhudiwa katika mji mkuu wa Khartoum kwa siku ya 20 mfululizo, na hivyo kudhoofisha juhudi za makubaliano ya kusitisha mapigano.

Ama kwa upande mwingine, mapigano makali yanayoendelea Khartoum yamevuruga juhudi za kupeleka misaada inayohitajika sana kwa raia waliokwama. Kuna wasiwasi mkubwa unaoongezeka kwa wale waliokwama na walioyakimbia mapigano. Wafanyakazi wa mashirika ya misada, pamoja na raia wamesema kuna uhaba wa huduma muhimu za msingi, huduma za afya, maji na chakula. Umoja wa Mataifa umeonya kuwa Wasudan wanakabiliwa na janga kubwa la kibinaadamu.

(AFP, DPA, AP, Reuters)