Hertha walenga kuwatuliza Bayern Munich | Michezo | DW | 27.11.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

Hertha walenga kuwatuliza Bayern Munich

Hertha Berlin wanalenga kuvunja kiu yao ya miaka 28 kupata ushindi dhidi ya Bayern Munich katika Bundesliga wakati watachuana katika ngome ya miamba hao wa Bavaria, Allianz Arena

Bayern wanaongoza msimamo wa ligi na tofauti ya pointi nane wakiwa na jumla ya pointi 37. Vijana hao wa Pep Guardiola wameshinda mechi zao zote saba nyumbani kwa takribani mabao manne au zaidi katika kila mechi na hawajashindwa mchuano wowote katika uwanja wa nyumbani msimu huu katika mashindano yote.

Hertha Berlin ambao sasa wanashikilia nafasi ya nne kwenye ligi, waliwashinda Bayern mbili bila kwa mara ya mwisho mnamo Oktoba 1977 lakini kocha wao Pal Dardai anasema hawana cha kuogopa anasema "Sasa tuko katika hali ambayo michezo yetu italinganishwa. Bayern ni timu bora ulimwenguni, nasi ni timu inayotia bidii sana. Tutaona pengo hilo ni kubwa kiasi gani. Udhaifu pekee ambao Bayern Munich iko nao ni kuwa upo wakati ambao watapoteza angalau pointi moja na hii ni fursa yetu sasa".

Borussia Dortmund ambao wako katika nafasi ya pili wanawaalika washika mkia Stuttgart kesho Jumapili ikiwa ni mchuano wa kwanza wa Sttugart baada ya kumtimua kocha Alexander Zorniger. Werder Bremen watakuwa nyumbani dhidi ya Hamburg hii leo katika debi ya kaskazini mwa Ujerumani.

Schalke 04 watakuwa wageni wa Bayer Leverkusen uwanjani Bay Arena kesho Jumapili huku kocha wa Schalke Andre Breitenreiter akiwa na shinikizo kubwa. Timu yake imeshindwa michuano yote saba ya mwisho katika mashindano yote. Timu zote zina pointi 20 kila mmoja, lakini tayari ziko pointi 17 nyuma ya viongozi Bayern. Katika mipambano mingine, Hanover 96 tapambana na Ingolstadt, Hoffenheim dhidi ya Bor. Moenchengladbach, Mainz 05 itakabana koo na Eintracht Frankfurt. Hapo kesho, Augsburg itafunga kazi dhidi ya Wolfsburg

Mwandishi: Bruce Amani
Mhariri: Josephat Charo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com