1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Havertz kukosa nusu fainali ya DFB Pokal

Deo Kaji Makomba
8 Juni 2020

Bayer Leverkusen inatarajia kutinga fainali ya kombe la shirikisho la Ujerumani, DFB Pokal, bila kiungo wake nyota Kai Havertz itakapokabiliana uso kwa uso na timu ya daraja la nne Saarbrucken Jumanne (09.06.2020).

https://p.dw.com/p/3dRqr
Bayer Leverkusen - FC Bayern München | Kai Havertz
Picha: Reuters/M. Hangst

Taarifa hiyo ya Kai Havertz kuikosa mechi dhidi ya Saarbrucken, imetolewa siku ya Jumatatu tarehe 08.06.2020 na kocha mkuu wa Leverkusen, Peter Bosz, ambaye alisema itakuwa ni mapema sana kwa mchezaji huyo kucheza hasa kutokana na jeraha linalomkabili kwa hivi sasa. Angeweza kucheza lakini kwa kufanya hivyo inaweza kumuhusisha mchezaji huyo na hatari fulani. Na hatutaki kuchukua jukumu la kumchezesha katika mechi hiyo," aliongeza kusema kocha Bosz.

Kiungo huyo mshambuliaji mwenye umri wa miaka 20 alikosa mechi ya Bundesliga Jumamosi (06.06.2020) wakati timu yake ilipokichafua na mabingwa watetezi Bayern Munich, na kisha kuambulia kichapo cha mabao 4-2, nyumbani, BayArena. Havertz, kwa hivi sasa anasumbuliwa na jeraha la msuli. Ni wazi kama atakuwa fiti, atateremka dimbani Jumapili ijayo wakati timu yake itakapokuwa shughuli na pevu mbele ya Schalke 04 ugenini Gelsenkirchen.

Leverkusen pia itamkosa nahodha wake Lars Bender, Daley Sinkgraven pamoja na Leon Bailey katika mechi ya nusu fainali ya kombe la shirikisho, lakini kocha Bosz anatarajia kuchagua kikosi imara kadri iwezekanavyo dhidi ya timu hiyo ya daraja la Nne, Saarbrücken, inayocheza katika ligi ya kanda ya kusini magharibi, Regionalliga Südwest.

"Hatutaitumia nusu fainali hii kuwapatia mafasi wachezaji ambao hawajafanya vyema," alisema Bosz. "Tunataka kutumia nusu fainali hii kufika fainali."

Nusu fainali nyingine ya DFB Pokal itwakutanisha vigogo wa soka Bayern Munich dhidi ya Eintracht Frankfut, mchezo utakaopigwa Jumatano tarehe 10.06.2020 huku fainali ya kombe hilo ikikung'utwa Julai 4 mwaka huu, huko mjini Berlin.

Deo Kaji Makomba/dpa