1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hatihati kwa M23 kuondoka kwenye maeneo wanayodhibiti

Daniel Gakuba
29 Machi 2023

Balozi wa Ufaransa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Bruno Albert amesema nchi yake inasubiri kuona kama waasi wa M23 wataondoka katika maeneo waliyoyakamata katika muda waliopewa.

https://p.dw.com/p/4PQZo
Konflikt im Kongo | M23 Soldaten
Picha: Guerchom Ndebo/AFP

Waasi hao wanatakiwa kuwa wameondoka katika maeneo waliyoyakamata ifikapo kesho Alhamisi ya tarehe 30 Machi, kabla ya kuchukua uamuzi juu ya vikwazo. Muda huo ndio wa mwisho waliowekewa waasi hao na makundi mengine yenye silaha wawe wameshaondoka katika maeneo waliyoyakamata. Duru kutoka Kinshasa zinaarifu kuwa waasi wa M23 ambao Kongo inaituhumu Rwanda kuwaunga mkono, bado wanadhibiti maeneo matatu muhimu katika mkoa wa Kivu Kaskazini. Aidha, msemaji wa muungano wa mashirika ya kiraia katika mkoa huo, Edgar Mateso ameiambia DW kuwa hakuna dalili za waasi wa M23 kuyahama maeneo wanayoyadhibiti na kuongeza kuwa badala yake wanaendelea kuyakamata maeneo mapya. Waasi hao wanadai azma yao ni kupata mazungumzo ya ana kwa ana na serikali ya Kinshasa.