Hamburg na Freiburg wasajili ushindi muhimu | Michezo | DW | 17.03.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Hamburg na Freiburg wasajili ushindi muhimu

Hamburg iliponea chupuchupu na kujiondoa katika kundi la timu tatu zinazoshika mkia kwa mara ya kwanza tangu Januari baada ya kusajili ushindi wa magoli mawili kwa moja nyumbani dhidi ya washika mkia Nuremberg

Huku Hamburg ikifanya kila iwezalo kuepuka shoka la kushushwa daraja, Mirko Slomka aliyechukua usukani kutoka kwa Bert van Marwijk kama kocha mwezi uliopita ameisaidia timu yake kusonga hadi nafasi ya 14.

Nuremberg wameshuka hadi nafasi ya 15 wakati VfB Stuttgart, waliotoka sare ya goli moja kwa moja na Werder Bremen siku ya Jumamosi chini ya mkufunzi Huub Stevens wakijikuta katika nafasi ya pili kutoka nyuma.

Eintracht Frankfurt walinyamazishwa na SC Freiburg ambao wamesonga katika nafasi ya 6

Eintracht Frankfurt walinyamazishwa na SC Freiburg ambao wamesonga katika nafasi ya 6

Freiburg walisonga hadi nafasi ya 16 kwenye msimamo wa ligi lakini bado wako katika kiticho cha kushushwa ngazi, licha ya kusajili ushindi wa mabao manne kwa moja dhidi ya Eintracht Frankfurt hapo jana.

Kileleni mwa ligi, viongozi Bayern Munich wanaweza kutawazwa mabingwa wa msimu huu Jumamosi ijayo, huku kukiwa na mechi nane msimu kukamilika. Hii ni baada ya ushindi wao wa mabao mawili kwa moja dhidi ya Bayer Leverkusen kuwapa uongozi wa pengo la pointi 23. Miamba hao wa Ulaya huenda wakapewa uchampioni kwa mara ya 24 kama watawabwaga Mainz nao mahasimu wao Borussia Dortmund na Schalke wote watoke sare. Kiungo wa Bayern Bastian Schweinsteiger ni mmoja wa waliotikisa wavu."Bila shaka kila kitu hakikwenda sawa, kwa sababu Leverkusen walikuwa wasumbufu sana. ulikuwa mchezo mgumu. Wakati mwingine unapaswa kuwa na uvumilivu kidogo. Labda haikuwa jioni nzuri ya kabumbu, lakini tulishinda mechi na hilo ndio jambo muhimu kabisa".

Leverkusen wako katika nafasi ya nne nyuma ya Schalke ambao waliwaadhibu Augbsurg mabao mawili kwa moja siku ya Ijumaa. Borussia Dortmund waliduwazwa kwa kichapo cha mabao mawili kwa moja na Borussia Moenchegladbach mapema Jumamosi. Dortmund sasa wako pointi moja mbele ya nambari tatu Schalke kabla ya mchuano wao wa utani wa Bonde la Ruhr mnamo Machi 25.

Vijana wa Jurgen Klopp, Dortmund waliona vimulimuli dhidi ya Gladbach

Vijana wa Jurgen Klopp, Dortmund waliona vimulimuli dhidi ya Gladbach

Kocha wa Gladbach Lucien Favre aliurefusha mkataba wake wiki iliyopita hadi mwaka wa 2017 na timu yake ilionyesha mchezo wa hali ya juu katika kipindi cha kwanza na kufunga magoli mawili katika dakika tisa. Huyu hapa kocha Lucien Favre. "Hatimaye tuna ushindi. Ulikuwa wakati mgumu. Ni wazi sote tumeridhika. Walitufanya kucheza kwenye mstari wa katikati. Walikuwa hatari sana kwa kuung'ang'ania mpira na kufanya mashambulizi ya kasi. Wakati mwingine tulizidiwa, tunahitaji kusema wazi, lakini tuliweza kupata mabao kwa wakati uliofaa".

FC Mainz ilisonga hadi nafasi ya tano baada ya kusajili ushindi mnono wa mabao manne kwa mawili dhidi ya Hoffenheim. Kocha wa Hoffenheim Martin Gisdol alisalia kujikuna kichwa tu baada ya kichapo hicho. "Ni vigumu kuelezea….Unapompa mpinzani magoli ya wazi. Tunapaswa kujilaumu sisi wenyewe kwa makosa yetu kutokana na mchezo mzuri tuliokuwa nao. Tungebidi kuwa mbele magoli hata matano kwa sifuri. Lakini tukafunga mbili tu….na katika Bundesliga hicho ni kishindo".

Mainz sasa wanaendelea kuwinda nafasi ya kucheza katika jukwaa la ulaya msimu ujao na wanapungukiwa na points tatu tu wakipata kibali cha kugaragaza soka la Champions League. Wolfsburg wamedondoka hadi nafasi ya sita baada ya sare ya goli moja kwa moja na washika mkia Eintracht Braunschweig. Matarijio ya Hertha Berlin kucheza Ulaya yaligonga mwamba baada ya kushindwa nyumbani mabao mawili bila jawabu mikononi mwa Hanover 96 na hivyo kusalia katika nafasi ya tisa.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/Reuters
Mhariri: Mohammed Khelef