Hali ya tahadhari Ukraine | Matukio ya Kisiasa | DW | 27.02.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Hali ya tahadhari Ukraine

Vikosi vya jeshi na polisi wa Ukraine Alhamisi (27.02.2014) vimewekwa kwenye hali kubwa ya tahadhari baada ya watu wenye silaha wanaoiunga mkono Urusi kuyateka majengo ya serikali na bunge katika mkoa wa Crimea.

Polisi wakilinda jengo la bunge kwenye mji wa Simferofol katika jimbo la Crimea.(27.02.2014).

Polisi wakilinda jengo la bunge kwenye mji wa Simferofol katika jimbo la Crimea.(27.02.2014).

Kiongozi wa mpito wa Ukraine leo amelionya jeshi la majini la Urusi lilioko Crimea kuvizuiwya vikosi vyake kwenye makambi baada ya watu wenye silaha wanaoiunga mkono Urusi kuyateka majengo ya serikali kwenye mji mkuu wa rasi hiyo wa Simferopol.

Kaimu Rais wa Ukraine Oleksandr Turchynov ameliambia bunge nyendo zozote zile za vikosi hivyo vitahesabiwa kuwa uvamizi wa kijeshi.Vikosi vya meli za kivita vya Urusi vina kambi yao katika mji wa Crimea wa Sevastopol.

Watu wenye silaha walionyakuwa majengo ya serikali huko Crimea wanadhaniwa kuwa ni wanachama wa makundi ya kujihami wenyewe ambayo yameibuka katika rasi hiyo ya Bahari Nyeusi baada ya kuangushwa kwa Rais Viktor Yanukovich mwishoni wa juma lililopita.Wamepandisha bendera za Urusi kwenye majengo hayo.

Waziri wa mambo ya ndani Arsen Avakov amekiita kitendo hicho kuwa uchokozi na amewaweka polisi na wanajeshi katika hali ya tahadhari.

Kitendo cha uchokozi

Vurugu baina ya wafuasi wa serikali ya Kiev na watu wenye kuiunga mkono Urusi katika mji wa Simferopol. Crimea.(26.02.2014).

Vurugu baina ya wafuasi wa serikali ya Kiev na watu wenye kuiunga mkono Urusi katika mji wa Simferopol. Crimea.(26.02.2014).

Avakov amesema kwenye mtandao wake wa Facebook kwamba wachokozi wanaadamana na kwamba wakati umefika wa kutuliza vichwa na kuchukuwa hatua makini. Kutekwa kwa majengo hayo kumekuja siku moja baada ya kuzuka mapambano huko Crimea jimbo linalojitegemea ambalo linaegemea upande wa Urusi kati ya watu wanaotaka kujitenga wanaoiunga mkono Urusi na wafuasi wa serikali mpya ilioko Kiev.

Bunge la Ukraine leo linatarajiwa kumchaguwa Arseniy Yatsenyuk ambaye alikuwa mtu muhimu katika maandamano yaliyomuangusha Rais Yanukovich kuwa waziri mkuu wa mpito wa Ukraine. Yatsenyuk mwenye umri wa miaka 39 akizungumza hapo jana baada ya kuteuliwa na mawaziri wenzake waliopendekezwa na viongozi walioongoza maandamano dhidi ya serikali ameelezea jinsi Ukraine ilivyo katika hali mbaya ya kifedha.

Hali ya maafa

Arseny Yatsenyuk aliyeteuliwa kuwa waziri mkuu wa mpito Ukraine.

Arseny Yatsenyuk aliyeteuliwa kuwa waziri mkuu wa mpito Ukraine.

Amesema" Tuko kwenye ukingo wa maafa na hii ni serikali ya watu wa kujiuwa kisiasa. Kwa hiyo karibu motoni."

Urusi imetangaza mazoezi ya kijeshi mpakani na Ukraine lakini waziri wa ulinzi wa Urusi Sergei Shoigun amesema mazoezi hayo kwa kiasi kikubwa hayahusiani na matukio yanayojiri Ukraine.

Mazoezi hayo yameshutumiwa na waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry ambaye amesema uingiliaji kati wa aina yoyote ule wa kijeshi nchini Ukraine litakuwa kosa kubwa.

Kuna hofu kubwa kwamba Ukraine iko kwenye ukingo wa kufilisika ambapo Kerry pia amesema serikali ya Marekani inaandaa udhamini wa mkopo wa dola bilioni moja pamoja na msaada mwengine wakati Umoja wa Ulaya inatafuta udhamini wa mkopo wa dola bilioni moja na nusu.

Mwandishi : Mohamed Dahman/ AFP/dpa

Mwandishi:Mohammed Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com