Hali ya kibinaadamu ni mbaya Sudan Kusini | Matukio ya Afrika | DW | 20.05.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Hali ya kibinaadamu ni mbaya Sudan Kusini

Vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyoendelea Sudan kusini vimesababisha janga la kibinaadamu. Hadi watu milioni mbili wanayakimbia mapigano na mashirika ya kutoa misaada yanaonya juu ya kutokea janga kubwa la kibinaadamu.

Mapigano makali yamezuka tena katika eneo la kaskazini la Sudan Kusini lenye utajiri mkubwa wa mafuta. Raia wanaoweza kukimbia wanalihama eneo hilo kuyanusuru maisha yao. Hata mashirika mengi ya kutoa misaada yameondoka eneo hilo na mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya mzozo wa Sudan Kusini Toby Lanzer amesema kwa kwa sababu hiyo watu takriban 500,000 hawana msaada.

Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa zaidi ya asilimia 50 ya wakazi milioni kumi na mbili wa Sudan Kusini wanahitaji msaada wa kibinaadamu.

Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu imethibitisha kwamba watoaji misaada wanaweza kuifikia idadi ndogo tu ya watu wanaohitaji msaada kwa dharura. Kukosekana msimu wa kupanda kutokana na vita kunazidisha hali kubwa mbaya, amesema Pawel Krzysiek, mfanyakazi wa shirika hilo katika mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba, wakati alipozungumza na DW.

"Wasiwasi mkubwa wa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu ni mustakabali wa raia. Tuko katika msimu wa mvua ambapo watu walitakiwa kupanda mazao yao ili baadaye waje kuvuna chakula chao, lakini shughuli zao za kilimo zimetatizwa."

Mateso dhidi ya watoto

Krzysiek amesema watoto ambao familia zao zimelazimika kuyakimbia mapigano ndio wanaokabiliwa na hali ngumu zaidi. Kamati ya Msalaba Mwekundu inasema watoto 250,000 wanakabiliwa na utapiamlo.

Afrika Bildergalerie Kindersoldaten im Süd-Sudan

Wanajeshi watoto Sudan Kusini

Umoja wa Mataifa umeonya kuhusu wimbi jipya la mateso dhidi ya watoto. Shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia watoto, UNICEF, limesema watoto kadhaa waliuwawa wiki iliyopita katika jimbo la Unity na makundi ya watu waliojihami na silaha. Watoto wengine walibakwa, kutekwa nyara au kusajiliwa kwa nguvu na kulazimishwa kujiunga na makundi ya wapiganaji.

Jonathan Veitch wa shirika la UNICEF amenukuliwa akisema baadhi ya washambuliaji ni watoto wa umri wa miaka 16. "Baadhi ya wapiganaji walieleza kwamba inafaa kuwaua watoto kabla wakue na kurejea kulipiza kisasi," alisema Veitch wakati wa mkutano kwa vyombo vya habari mjini Geneva kupitia simu akiwa mjini Juba. Umoja wa Mataifa unakadiria watoto 13,000 wamesajiliwa kuwa wapiganaji na pande zote mbili za mzozo wa Sudan Kusini.

Hospitali hatarini

Katika eneo la Kodok kaskazini mwa Malakal Shirika la Msalaba Mwekundu linadhimini hospitali. Lakini kutokana na mapigano yanayoendelea limelazimika kupunguza shughuli katika hospitali hiyo.

"Kutokana na mapigano tulilazimika kuondoa sehemu ya wafanyakazi wetu kutoka eneo hilo na kuwapeleka katika eneo lililo salama. Huo ni uamuzi mkubwa usiotarajiwa kwa sababu hospitali hii ni muhimu sana kwa otoaji wa huduma za afya kwa watu wa eneo hili," alisema Krzysiek.

DW Afrika Kodok Krankenhaus

Hospitali ya Kodok

Takriban wagonjwa 600 walikuwa wakipokea matibabu katika hospitali hiyo kila wiki, hususan watoto. "Athari zaidi zinatarajiwa kushuhudiwa wakati vita vitakapomalizika ghafla na msaada wa kimataifa utakapopunguzwa kwa kiwango kikubwa," ameongeza kusema Pawel Krzysie. Anafahamu fika kuwa hilo halitatokeo kwa haraka.

Wakati mashirika ya misaada yakiendelea kuhimiza amani ili yaweza kusambaza misaada kwa raia, serikali ya Sudan Kusini ilipokea silaha za za thamani ya dola milioni 38 mwaka jana kutoka kwa China ambazo imezilipia kutumia mafuta.

Ukiukaji mkubwa wa haki za binaadamu

Jeshi la Sudan Kusini limenyoshewa kidole cha lawama kwa ukiukaji mkubwa wa haki za binaadamu wakati wa operesheni yake ya kupambana na waasi iliyoanza mwishoni mwa mwezi uliopita katika jimbo la kaskazini la Unity na kuenea katika majimbo ya Jonglei na Upper Nile. Katika tangazo lake Shirika la Maendeleo la Mashariki na Pembe ya Afrika, IGAD, lilisema jeshi hilo liliwapiga raia, kuviharibu vijiji na kufanya vitendo viovu na visivyokubalika.

Shirika la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch limesema vyombo vya usalama vya Sudan Kusini vinazikanyaga haki za binaadamu katika operesheni zao. Leslie Lefkow, afisa wa shirika hilo mjini Abidjan nchini Cote d'Ivoire amesema wafungwa wanazuiwa na kuteswa bila kutambuliwa Sudan Kusini.

Symbolbild - Soldaten Südsudan

Wanajeshi wa Sudan Kusini

"Shirika la Human Rights Watch limeorodhesha matukio kadhaa ambapo jeshi na idara ya usalama ya kitaifa wamewazuia na wakati mwingine kuwatesa wafungwa katika mwezi uliopita. Udhalilishaji huu unafanyika wakati kukiwa na mashambulizi dhidi ya raia yanayofanywa na pande zinazopigana Sudan Kusini."

Leslie amesema mbali na vita vinavyoendelea ni muhimu pia kufanyike mageuzi ya sheria Sudan Kusini ili kudhibiti mamlaka ya jeshi na vyombo vya usalama. Msemaji wa jeshi la Sudan Kusini Philip Aguer amekanusha madai yote ya ukiukaji wa haki za binaadamu, akisema jeshi linajilinda na kufuata utaratibu wa kutowashambulia raia.

Mwandishi:Cascais, Antonio (HA Afrika)

Tafsiri:Josephat Charo

Mhariri:Iddi Ssessanga