Hali Tete Msumbiji | Matukio ya Afrika | DW | 19.06.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Hali Tete Msumbiji

Watu 39 wameua na wengine 1000 kupoteza makaazi kwenye mashambulio yaliyotekelezwa na makundi yaliyojihami katika mkoa wa kaskazini wa Msumbiji wa Cabo Delgado tangu mwezi Mei mwaka 2018, limesema Human Rights Watch.

Shirika hilo la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch linasema kuwa mamia ya familia zimetoroka vijiji vyao baada ya wanachama wa makundi yanayodaiwa kuwa ya Kiislamu kuteketeza nyumba zao kwenye mashambulio ya usiku.

Watafiti wa Shirika la Human Rights Watch walizuru kijiji cha Naunde, kilichoko mjini Mucojo, katika wilaya ya Macomia baada ya shambulio lililofanywa mwezi Juni tarehe tano na kushuhudia nyumba 164, magari matano na maelfu ya mifugo walioteketezwa.

Wakaazi wanatoroka vijijini

Wakaazi walisema kuwa waliotekeleza kitendo hicho walichoma pia msikiti, ikiwemo nakala za Quran na mikeka ya swala na kumchinja kiongozi wa kiislamu ndani ya msikiti huo. Aidha watafiti hao waliona watu wengine wakibeba virago vyao huku wakitoroka kijiji hicho.

Shirika la Human Rights Watch pia lilizungumza na wakaazi wa kijiji ambacho kilishambuliwa kwenye kisa cha hivi karibuni cha mwezi Juni tarehe sita tarehe 12. Duru kadhaa katika wilaya za Macomia na Quissanga zilithibitisha kuwa watu walikuwa wangali wanatoroka kwa hofu ya mashambulio zaidi.

Mashambulio yameathiri wanawake na watoto, Msumbiji

Mashambulio yameathiri wanawake na watoto, Msumbiji

Mwanakijiji mmoja katika kijiji cha Naunde alisema kuwa walioshambulia walimkamata kiongozi wa kijiji. "Alipogundua kuwa walikuwa wakimtafuta, alijaribu kutoroka lakini mmoja wao alimkamata na kumkata kichwa mbele ya watu.”

Msururu wa mashambulio katika mkoa wa Cabo Delgado ulianza mwezi Oktoba mwaka 2017, wakati kikundi kilichojihami kinachotuhumiwa kuwa cha waislamu kuvamia vituo kadhaa vya polisi katika wilaya ya Mocimboa da Praia, na kusababisha hofu na ujio wa wanajeshi wengi.

Baada ya shambulio hilo, mamlaka nchini Msumbuji yalifunga misikiti saba na kuwazuia zaidi ya watu 300 bila ya kuwashtaki, wakiwemo viongozi wa dini na wageni ambao wanasemekana kuwa na mahusiano na mashambulio katika wilaya za Palma na Mocimboa da Praia. Ian Levin anahudumu na shirika la Human Rights Watch anasema, "Kuna suala la haki za binadamu ambalo ni muhimu kwa uthabiti na utajiri wa muda mrefu kwa taifa la Msumbiji. Ni muhimu kwa serikali kufanya uchunguzi kwa vyombo vyake vya usalama kwa njia huru."

Vyombo vya usalama vinakiuka haki za binadamu

Wanajeshi waliotumwa katika mji wa Mucojo baada ya shambulio katika kijiji kilichoko karibu cha Naunde wameliambia shirika la Human Rights Watch kwamba, tangu mwezi Aprili, wamewatia nguvuni zaidi ya watuhumiwa 200 walio na mahusiano na makundi yanayotekeleza mashambulio na kuwakabidhi kwa maafisa wa polisi. Wanajeshi hao walisema kuwa watuhumiwa hao walikataa kufichua nia yao ya kutekeleza mashambulio ama hata kutaja majina ya viongozi wao.

Rais Filipe Nyusi akimsalimu kiongozi wa upinzani Afonso Dhlakama 2015

Rais Filipe Nyusi akimsalimu kiongozi wa upinzani Afonso Dhlakama 2015

Vyombo vya usalama nchini Msumbiji vina makubaliano na Shirika la Kimataifa linaloshughulikia haki za wanasiasa na kupinga mateso dhidi ya watu wanaozuliwa pamoja na mikataba mingine ya kimataifa ambayo Msumbiji imesaini.

Makubaliano hayo yanazuia mauaji ya kiholela na mateso dhidi ya watu wanaoshikiliwa. Watuhumiwa wanaozuiliwa wanastahili kushtakiwa na kuhukumiwa mbele ya jaji haraka iwezekanavyo ama kuachiwa huru.

Kikundi kinachotuhumiwa kutekeleza mashambulio hayo kinaitwa Al-Sunna wa Jama'a na Al-Shabab, lakini hakuna ushahidi wa kuvihusisha na kikundi kama hicho nchini Somalia. Wanaharakati nchini humo wameliambia shirika la Human Rights Watch kuwa zaidi ya nyumba 400 zimeteketezwa katika kipindi cha majuma mawili yaliyopita na kuwafanya watu kupoteza makaazi katika wilaya tatu.

Mwandishi: Shisia Wasilwa, https://www.hrw.org/africa/Mozambique

Mhariri: Josephat Charo