1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali nchini Iraq

15 Agosti 2011

Zaidi ya watu 75 wamepoteza maisha yao katika mashambulio chungu nzima ya mabomu yaliyoitikisa miji kadhaa ya Iraq hii leo.Mashambulio hayo yanatokea huku wanajeshi wa Marekani wakijiandaa kuihama Irak.

https://p.dw.com/p/12Grc
Wanajeshi wa IrakPicha: DW

Idadi hiyo ya wahanga ambayo ni ya awali,imepindukia idadi ya wahanga pale makomando wa Al Qaida walipolivamia baraza la mkoa wa Salaheddine huko Tikrit,Marxch 29 mwaka huu ambapo watu 58 walipoteza maisha yao.

Iliyoshambuliwa hii leo ni pamoja na miji ya Kout,Tikrit,Baghdad,Taji,Najaf,Kirkouk,Ramada,Kerbala,Khan Beni Saad,Iskandariya,Mosoul,Balad na mitaa chungu nzima ya mkoa wa Diyala,ikiwa ni pamoja na Baqouba .

Katika taarifa yake spika wa bunge la Iraq,Iyad al Oussama al-Noujaifi amelaani mashambulio hayo aliyoyataja kuwa ni ya kinyama.

"Nnataka kujua sababu ya mashambulio haya na nani wako nyuma" amesema spika wa bunge na kushadidia umuhimu wa kuimarishwa juhudi ili kuepusha balaa kama hilo.

Irak Kirkuk Attentat Anschlag Autobombe Flash-Galerie
Shambulio la bomu huko KirkukPicha: picture alliance / dpa

Shambulio baya zaidi lililitokea Kout,umbali wa kilomita 160 kusini mashariki ya mji mkuu Baghdad ambako kwanza bomu liliripuliwa katika uwanja wa mji huo uliosheheni watu na baadae gari lililotegwa miripuko kuripuka wakati vikosi vya usalama vilipofika katika eneo hilo.Watu 40 wamepoteza maisha yao na zaidi ya 68 kujeruhiwa.

Mashamabulio haya ya mabomu yanajiri kati kati ya mwezi mtukufu wa Ramadhan na katika wakati ambapo maakundi muhimu ya kisiasa nchini Iraq yamefikia makubaliano ya kuiruhusu serikali ijadiliane na Marekani kuhusu kuendelea kuwepo nchini humo idadi ndogo ya washauri wanaotoa mafunzo ya kijeshi,hata muda wa kuhamishwa wanajeshi wa Marekani utakapowadia mwishoni mwa mwaka huu.

Parlamentseröffnung im Irak
Bunge la IrakPicha: AP

Wanajeshi 47 wa kimarekani bado wangalipo nchini Iraq-na kwa mujibu wa makubaliano ya usalama yaliyotiwa saini November mwaka 2008 kati ya Baghdad na Washington,wote hao wanabidi waihame Irak hadi mwisho wa mwaka huu.

Lakini pande zote mbili,tangu wamarekani mpaka wairaq,wanatambua,kutiwa saini makubaliano tu haitoshi.KUna masuala kadhaa yanahitaji kupatiwa majibu kuhusu idadi ya wanajeshi,muda na masharti ya kuendelea kuwepo kwao nchini Iraq.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters/Afp

Mhariri:Josephat Charo