1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Madagascar | Suche nach Wasser
Picha: Laetitia Bezain/AP/picture alliance

Hali mbaya ya ukame yaziathiri nchi nyingi za Afrika

13 Mei 2021

Kiwango kisicho cha kawaida cha ukame katika nchi nyingi za afrika kimewaacha wataalam na mashirika ya misaada katika wasiwasi mkubwa wa kitisho cha baa la njaa. 

https://p.dw.com/p/3tKvq

Wakati janga la covid 19 likiendelea kuyaathiri mataifa mengi, shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP, limeonya kwamba nchi nyingi hivi karibuni zitakabiliwa na baa la njaa kutokana na ukame uliokithiri.

Eneo la kusini mwa Madagascar kwa hivi sasa linakabiliwa na mgogoro mbaya wa njaa uliochangiwa na ukame na dhoruba za mchanga ambavyo vimesababisha ardhi kukosa rutuba. Hali imekuwa mbaya hata nzige ambao kwa kawaida wanachukuliwa kama kitisho cha mazao, sasa wamekuwa tegemeo la wananchi wengi ambao wanawala kama chakula.

Mkulima mmoja wa nchini humo Najoro anaeleza kwamba "hatujavuna kitu kwa karibu miaka miwili", akiongeza kuwa bila ya nzige, basi wangekuwa wamepoteza maisha.

BG Wasserverbrauch Anbauprodukte Afrika | Hirse in Simbabwe
mazao mengi yamo katika kitisho kwa sababu ya ukamePicha: Getty Images/AFP/J. Njikizana

Watoto ndio wamekuwa wahanga wakubwa. Ujumbe wa misaada wa WFP katika mji wa Tranomaro umekuwa ukikabilana na ongezeko la vifo vya watoto vinavyotokana na utapiamlo. Shirika hilo la WFP limekuwa likisambaza msaada wa chakula. Amer Daoudi, mkurugenzi mwandamizi wa operesheni katika WFP alisema kwamba hali ni mbaya sana na kwamba "baa la njaa linanyemelea eneo la kusini mwa Madagascar.

Wakati huohuo nchini Zimbabwe, ukame wa miaka mingi umeifanya nchi hiyo kukosa usalama wa chakula. Mwanzoni mwa mwaka huu, WFP ilitabiri kwamba takribani watu milioni 7.7 kati ya idadi jumla ya watu milioni 15 watahitaji msaada wa chakula katika nusu ya kwanza ya mwaka.

Nchi jirani ya Angola, pia inahangaika na hali mbaya ya ukame angalau kwa miongo minne. Wakati matatizo ya kilimo nchini Zimbabwe yanahusishwa na mpango wake wa mageuzi mwanzoni mwa mwaka 1980, uzoefu wa Angola unathibitisha kwamba masuala yanayohusiana na ukame yanakwenda mbali zaidi ya umiliki wa ardhi.

Nchini Angola pia, WFP inaonya juu ya kitisho cha mgogoro wa njaa, pamona na ukosefu wa chakula wa muda mrefu  na utapiamlo katika maeneo yaliyoathiriwa vibaya.Wakati usambazaji wa maji ukiendelea kupungua, karibu asilimia 40 ya mazao yameharibika na mifugo ipo hatarini. Ongezeko la kitisho cha kukosekana usalama wa chakula, pia kumechangia kiwango kisicho cha kawaida cha uhamiji.

Südafrika Global Ideas | The Karoo
Picha: Henner Frankefeld/DW

Familia nyingi sasa zinatoka maeneo yaliyoathirika na kuhamia katika mikoa mingine na katika maeneo ya karibu na mpaka na Namibia. Baadhi ya maeneo ya Namibia nayo yameshuhudia ukame. Zimbabwe ilitangaza kwamba inatarajia mavuno mazuri ya nafaka katika nusu ya mwaka huu kufuatia msimu mzuri wa mvua.

Mkulima kama Xvier Tawasika anatiwa moyo na matarajio hayo ya mavuno akisema, "mwaka 2021 umekuwa mzuri ukilinganisha na miaka iliyopita". Tawasika anatarajia kuvuna nafaka za ziada zitakazosaidia familia yake hadi msimu ujao wa mavuno. Serikali ya Zimbabwe imekuwa na msimamo kwamba nchi ipo katika nafasi nzuri ya kukabiliana na kitisho chochote  katika sekta ya kilimo ukilinganisha na miaka iliyopita.

Zimbabwe ilianza kuwekeza kwenye miradi ya kilimo ambayo inaendana na mabadiliko ya tabia nchi. Naibu waziri wa kilimo Vangelis Haritatos, anadai kwamba mwelekeo wa nchi hyo umeanza kuwa na matokeo chanya. Miongoni mwa njia endelevu za kilimo zilizotumika ni pamoja na kuimarisha mfumo wa kilimo cha umwagiliaji na kuvuna maji sambamba na kuwahamasisha wakulima wapande nafaka zinazostahimili ukame.