1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali kuwa mbaya zaidi Syria ifikapo mwakani

9 Novemba 2012

Umoja wa Mataifa umeonya kuwa idadi ya wakimbizi wa ndani wanaohitaji misaada ya kibinaadamu nchini Syria itafikia milioni nne kutoka milioni mbili na nusu ya sasa endapo mauwaji hayatasitishwa.

https://p.dw.com/p/16fu4
UN-Sicherheitsrat 2011Picha: AP

Mkurugenzi wa ofisi ya umoja huo inayoshughulika na masuala ya kiutu John Ging amesema kuwa kushindwa kusitisha mauwaji hayo pia kutasababisha kuongezeka kwa wimbi la wakimbizi wanaokimbilia mataifa ya jirani kutoka 400,000 kwa sasa na kufikia 700,000 mwanzoni mwa mwaka ujao wa 2013.

Ging ameyasema hayo kabla ya kuanza kwa mkutano wa tano wa huduma za kiutu kwa watu wa Syria unaofanyika Geneva, Uswis na ambao utahudhuriwa na wawakilishi zaidi ya 350.

Rais Bashar al-Assad wa Syria
Rais Bashar al-Assad wa SyriaPicha: AFP/Getty Images

Hapo jana Rais Assad alitoa kauli akiweka bayana kuwa kamwe hatatoa mguu wake nje ya Syria na kwamba ataishi humo siku zote na atakufa akiwa humo na kuonya kuwa hatua yoyote ya kuivamia nchi yake itaigharimu dunia nzima.

"Gharama ya uvamizi huo kama utafanyika itakuwa kubwa sana kuliko dunia inavyoweza kuimudu kwa sababu kama una matatizo ndani ya Syria na sisi ndio ngome pekee imara iliyosalia ya mfumo usio wa kidini na yenye utulivu katika eneo zima la mashariki ya kati. Kama utafanyika, utakuwa na athari ambazo zitaiathiri dunia kuanzia Antlantic hadi Pasific. Sifikirii kama mataifa ya magharibi yana mwelekeo huo lakini kama yanayo hakuna anayeweza kusema kitakachofuata" alisema Assad

Akizungumza na kituo cha televisheni cha Urusi, RT, kwa lugha ya kiingereza Assad amesema " mimi sio kibaraka. Sikuzaliwa magharibi ili nikaishi huko au hata nchi nyingine yoyote. Mimi ni Msyria, nimezaliwa Syria, ninatakiwa kuishi na kufia hapa."

Machafuko nchini Syria
Machafuko nchini SyriaPicha: REUTERS

Wakati Assad akiyasema hayo wapinzani wake wanaoishi nje ya nchi wanaendela na majadiliano huko Doha juu ya namna ya kumtoa madarakani.

Kiongozi wa kundi hilo Hytham al-Maleh amesema kuwa wana matumaini watafikia makubaliano hii leo baada ya Baraza la Kitaifa la Syria, SNC, kufanikiwa kuchagua uongozi mpya.

Mpango wa upinzani ni kuungana kuwa na nguvu ambayo itaruhusu kuratibu hatua ya kutumika nguvu za kijeshi dhidi ya utawala wa Assad, kuziweka kanda za kiutawala chini ya imaya yao pamoja na kuwezesha huduma za kibinaadamu kuwafikia wenye mahitaji.

Wapinzani wa Assad Syria
Wapinzani wa Assad SyriaPicha: Reuters

Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ambayo ndiyo inaratibu mkutano Ahmed ben Helli amewaambia waandishi wa habari kuwa washiriki wamepewa wito kutatua changamoto kuu zinazowasababisha kushindwa kumng´oa Assad madarakani.

Mwandishi: Stumai George/ AFP/AP

Mhariri: Yusuf Saumu