1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali kisiwani Madagascar

Oumilkher Hamidou20 Februari 2009

Wizara zakombolewa na vikosi vya usalama

https://p.dw.com/p/Gxx2
Meya wa zamani wa Antananarivo Andry RajoelinaPicha: AP


Vikosi vya usalama vya Madagascar vimezikomboa bila ya matumizi ya nguvu leo asubuhi,wizara nne zilizokua zikishikiliwa tangu jana na wafuasi wa meya wa mji mkuu ANTANANARIVO,aliyepokonywa cheo chake, Andry Rajoelina.



Vikosi vya usalama vinapiga doria katika maeneo yanayozizunguka wizara hizo tangu vilipoingilia kati kuwatimua wafuasi wa Andry Rajoelina jana usiku.


Kwa mujibu wa mashahidi,milio ya hapa na pale ya risasi ilisikika alfajiri ya leo katika mtaa mashuhuri wa mji mkuu zinakokutikana wizara zote za serikali.Hali inasemekana ni shuwari kwa sasa.


"Wizara zilizokua zikishikiliwa na upande wa upinzani zimeshakombolewa na vizuwizi vimeshaondolewa.Watumishi wa serikali wanaweza kurejea kazini" amesema hayo waziri wa usalama wa ndani ,Desiré RASOLOFOMANANA kupitia televisheni ya taifa hii leo.


Wizara yake ilikua miongoni mwa nne zilizokua zikishikiliwa na wafuasi wa Rajoelina,meya wa zamani wa mji mkuu Antananarivo,anaeongoza vugu vugu la upinzani dhidi ya rais Marc Ravalomanana.


Watu wasiopungua 50 wamekamatwa na polisi .Katika wakati ambapo mvutano katika kisiwa cha Bukini umeshagharimu maisha ya watu 125 tangu uliporipuka january 26 iliyopita,juhudi za upatanishi zimeshika kasi kisiwani humo.Wapatanishi wamesema rais Marc Ravalomanana amekubali kukutana na Andry Rajoelina.


Wakati huo huo rais Marc Ravalomanana anaelaumiwa na mpinzani wake Anmdry Rajoelina kutawala kimabavu,amemchagua waziri mwengine wa mambo ya ndani,kutokana na kile rais alichokiita "sababu za afya za Gervais RAKOTONIRINA."


Kwa mujibu wa taarifa ya ofisi ya rais,mabadiliko hayo ya serikali yamesababishwa na "umuhimu wa wizara hiyo katika kudhamini ipasavyo usalama wa taifa."


Itafaa kusema hapa kwamba Gervais RAKOTONIRINA amechaguliwa mapema mwezi uliopita kuongoza wizara ya ndani ambayo kabla ya hapo ilikua ikidhibitiwa na waziri mkuu.


Rais Marc Ravalomanana amemchagua hivi sasa mkuu wa zamani wa vikosi vya polisi katika mji mkuu,Rabenja Sehenoarisoa kua waziri waziri wa mambo ya ndani