Hali inatisha Sudan Kusini | Matukio ya Afrika | DW | 17.01.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Hali inatisha Sudan Kusini

Maelfu ya wakaazi wa Sudan Kusini wanayapa kisogo maskani yao kufuatia mapigano. Waasi wanashikilia Uganda iache kuwaunga mkono wanajeshi wa serikali la sivyo hawatotia saini makubaliano ya kuweka chini silaha.

Vikosi vya serikali vinapigania mji wa Malakal

Vikosi vya serikali vinapigania mji wa Malakal

Mazungumzo ya amani yanayosimamiwa na jumuiya ya ushirikiano na maendeleo IGAD katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Abeba, yanazorota. Waasi wanaoongozwa na makamo wa rais wa zamani, Riek Machar, wanashikilia ili makubaliano ya kuweka chini silaha yatiwe saini, kwanza Uganda iache kuwasaidia wanajeshi wa serikali ya rais wa Sudan Kusini, Silva Kiir.

Alikuwa rais Yoweri Museveni binafsi aliyekiri kwa mara ya kwanza kabisa Jumatano iliyopita kwamba anamsaidia kijeshi kiongozi mwenzake wa Sudan Kusini katika mapambano yanayoendelea tangu mwezi mmoja sasa dhidi ya makamo wake wa zamani wa rais, Riek Machar.

"IGAD imeshapokea malalamiko yetu, kuingilia kati vikosi vya kigeni kunazidi kukorofisha mzozo na ingekuwa jambo la maana wangeondoka," amesema Mabior Garang, mmojawapo wa wasemaji wa ujumbe wa waasi mazungumzoni.

Mjumbe mmoja wa serikali ya mjini Juba ambaye hakutaka jina lake litajwe amezungumzia mkataba wa ushirikiano wa kijeshi kati ya nchi yake na Uganda akisisitiza tunanukuu "ushirikiano huo umejadiliwa kati ya nchi mbili tu na sio pamoja na kundi la waasi. "Mwisho wa kumnukuu.

Maelfu wameuwawa

Südsudan Kämpfe 28.12.2013

Majeruhi wanatibiwa

Mapigano yaliyoripuka tangu katikati ya mwezi wa Desemba mwaka jana kutokana na uhasama wa kikabila yameshaangamiza maisha ya watu wasiopungua elfu kumi. Mauwaji ya kikatili yanaripotiwa kutokea nchini humo.

Afisa wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa amesema jana wameona maiti za raia wa kawaida waliofungwa mikono na miguu kabla ya kuuliwa.

Pande zote mbili, tangu kambi ya rais Salva Kiir mpaka ile ya hasimu yake Riek Machar zinalaumiwa kuhusika na visa vya kikatili nchini humo.

Katika wakati ambapo Umoja wa Mataifa umeahidi kufanya uchunguzi kuhusu visa vya uhalifu dhidi ya ubinaadamu, naibu katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia masuala ya haki za binaadamu, Ivan Simmonovic, anasema wachunguzi 92 wameshafika nchini humo. Ripoti yao ya kwanza inatarajiwa kuchapishwa wiki mbili kutoka sasa.

Ripoti iliyochapishwa jana na shirika la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch inazungumzia juu ya "uhalifu uliokithiri" dhidi ya raia kwa sababu za kikabila."

Mapigano yanayoendelea Sudan Kusini yamepelekea maelfu kuyapa kisogo maskani yao. Shirika la Umoja wa mataifa linalowahudumia wakimbizi, UNHCR, linasema watu wasiopungua elfu 80, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, wameyapa kisogo mapigano hayo hadi sasa.

Maelfu wanayapa kisogo maskani yao

Südsudans Präsident Salva Kiir Mayardit

Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini

Katika kambi za Umoja wa Mataifa huko Juba, kasisi Jacob Thelekkadan ni miongoni mwa wale wanaowashughulikia wakimbizi wa ndani. Akizungumza na DW, kasisi Jacob Thelekkadan anazungumzia hali ya wakimbizi hao walipofika kambini.Anasema"Wanakuwa wamechoka kupita kiasi. Watu wameingiwa na wasiwasi wanahofia mauwaji ya kulipiza kisasi na maovu mengineyo. Ndio maana wanaona bora kuyahama maskani yao na kuja katika mahala salama ingawa hakuna maji wala chakula cha kutosha lakini angalao kuna usalama hapa katika kambi za Umoja wa mataifa."

Ripoti za hivi punde zinasema jeshi la serikali limetangaza kushindwa kuwasiliana na wanajeshi wake huko Malakal - ushahidi kwamba mji huo umeangukia mikononi mwa waasi.

Mwandishi: Hamibou Oummilkheir/AFP/Reuters

Mhariri: Josephat Charo