Hali inatisha nchini Tchad | Matukio ya Kisiasa | DW | 01.02.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Hali inatisha nchini Tchad

Waasi wanatishia kuuvamia mji mkuu Djamena katika wakati huu ambapo umoja wa Ulaya unapanga kutuma wanajeshi wake nchini Tchad

default

Mkuu wa vikosi vya Umoja wa Ulaya nchini TchadWakaazi wa Ndjamena,wanahofia mapigano yasije yakaripuka wakati wowote kutoka sasa katika mji mkuu huo,baada ya kuripuka leo asubuhi umbali wa kilomita 50 tuu kati ya waasi wanaompinga rais Idris Deby na wanajeshi wa Tchad.


Baada ya ripoti kwamba waasi wamekua wakisonga mbele tangu siku tano zilizopita kuelekea mji mkuu Ndjamena,bila ya kukutana na upinzani wowote,mapigano makali yameripotiwa hii leo katika njia inayounganisha eneo la mashariki ya Tchad na Ndjamena-umbali wa kilomita 50 karibu na mji mkuu huo.


Mapigano hayo  yalisita lakini muda mfupi baadae bila ya kujulikana kwa manufaa ya nani.Uongozi wa kijeshi wa Tchad unadai unaendelea kuwaandama waasi huku mkuu mmojawapo wa muungano wa makundi matatu ya waasi wa Tchad,Timan Erdimi akihoji wamewatimua wanajeshi wa serikali.Waasi wanasema wameshaingia karibu na mji wa Massaaguet tangu mchana na wanaahidi kuingia Ndjamena wakati wowote kutoka sasa.


"Mapambano makubwa yatashuhudiwa Ndjamena" amesisitiza Timan Erdimi,ambae jana alimpa muda rais Idris Deby wa Tchad aanzishe mazungumzo ya kugawana madaraka .


Wakaazi wa mjini Ndjamena wameingiwa na hofu,kama bibi huyo anavyosema:


"Hali inatia wasi wasi,inatia hatarini juhudi zote.Wahenga wanasema vita havina maana.Wanabidi waanzishe mazungumzo.Watu wameshaanza kujinunulia vyakula-hali inatisha kweli kweli."


Tangu saa 24 zilizopita hali inatisha mjini Ndjamena ambako mawasiliano ya simu yamevurugika kutokana na ukosefu wa umeme.


Shughuli za usafitri zimepooza na idadi ya wanajeshi wanaopiga doria imeongezeka mjini Ndjamena.Majumba ya serikali yanalindwa.


Serikali ya Ufaransa imetuma wanajeshi zaidi ya elfu moja kusaidiana na wenzao walioko nchini Tchad ili-kama wizara ya ulinzi ilivyosema mjini Paris- kudhamini usalama wa raia wa kifaransa.


Mashambulio haya makubwa kabisa kuwahi kushuhudiwa ya waasi yanajiri katika wakati ambapo Umoja wa Ulaya unajiandaa kutuma  nchini Tchad wanajeshi 3700 wa kikosi cha EURFOR ,hadi mwezi May ujao, kwa lengo la kuwalinda wakimbizi wa Darfour na wakaazi wa Tchad na Jamhuri ya Afrika kati walioyapa kisogo maskani yao.Karibu nusu ya wanajeshi hao ni wa kutoka Ufaransa.


Habari kutoka Bruxelles zinasema opereshini ya kuwasafirisha wanajeshi wa Austria na Irlande waliokuwa waelekee Tchad hii leo imeakhirishwa kutokana na hali namna ilivyo nchini Tchad.


"Safari tatu za ndege,moja ikiwa na dazeni moja ya wanajeshi wa Austria na mbili zikiwa na wanajeshi 50 wa Ireland na vifaa vya kijeshi zimeakhirishwa kwasababu ya mapigano kati ya vikosi vya waasi na wanajeshi wa serikali ya Tchad."amesema hayo msemaji wa opereshini  za EURFOR karibu na Paris luteni kanali Philippe de Cussac hii leo.Ameongeza kusema hata hivyo wanafuatilizia kwa makini hali namna ilivyo.


Nalo shirika la Umoja wa mataifa linalowahudumia wakimbizi UNHCR limeamua kuwahamishia Kameroun watumishi wake kutoka Ndjamena.

►◄

 • Tarehe 01.02.2008
 • Mwandishi Hamidou, Oumilkher
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/D158
 • Tarehe 01.02.2008
 • Mwandishi Hamidou, Oumilkher
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/D158

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com