Hali ilivyo Kyrgyzstan. | Matukio ya Kisiasa | DW | 18.06.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Hali ilivyo Kyrgyzstan.

Wakati hali ikiwa bado si shwari nchini Kyrgyzstan, kiongozi wa muda wa nchi hiyo, Roza Otunbayeva, amefanya ziara katika eneo la kusini mwa nchi hiyo linalokabiliwa na mapigano, na kuahidi kuujenga tena.

default

Rais wa mpito wa Kyrgyzstan, Roza Otunbayeva.

Rais huyo wa mpito wa Kyrgyzstan, Bibi Roza Otunbayeva, aliwasili leo katika mji wa Osh kwa helikopta ya kijeshi kwa lengo la kukutana na viongozi wa eneo hilo, ambapo katika mitaa mbalimbali ya mji huo alijionea majengo yaliyoharibiwa kutokana na ghasia zilizotokea.

Taarifa ya serikali ilimnukuu Bibi Otunbayeva akielezea nia ya kuujenga tena mji huo wa Osh, kwa hali yoyote ile, ili kuwezesha watu waliokimbia kurudi katika nyumba zao.

Serikali ya nchi hiyo ilikuwa ikijitahidi  kurudisha utulivu kufuatia mapigano kati ya wakazi wenye asili ya Uzbek na wale wa Kyrgyz, ambayo yalisababisha vifo vya watu 200 wikli iliyopita, ghasia ambazo zimeelezwa kuwa ni mbaya kabisa kuwahi kutokea nchini humo katika kipindi cha miongo miwili iliyopita.

Hata hivyo, idadi ya watu waliokufa imeelezwa kuwa inaweza kuwa zaidi ya hiyo huku takriban wat 2,000 wakijeruhiwa.

Maelfu ya wakimbizi waliotokana na mapigano hayo, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, wamekusanyika katika makambi ya muda ambayo mengi yanakabiliwa na uhaba wa maji na chakula.

Rais wa muda wa Kyrgyzstan, Roza Otunbayeva, ambaye serikali yake bado haijachaguliwa rasmi, amemtuhumu aliyekuwa Rais wa nchi hiyo,  Kurmanbek Bakiyev, kwa kuandaa magenge ya watu wenye silaha kufanya ghasia katika eneo hilo la kusini, ambalo ni ngome yake kubwa, kwa kuchochea ugomvi wa kikabila kati ya Wa-Uzbeks na Wakyrgyz.

Kyrgyzstan, nchi ambayo ilikuwa katika muungano wa Sovieti, wa iliyokuwa Urusi ya zamani,  ilikumbwa na machafuko  toka kutokea kwa uasi mwezi April, ambapo Rais Bakiyev alipinduliwa na serikali ya mpito kushika madaraka.

Tangu kuanza kwa wiki hii, ghasia katika mji huo wa Osh zimepungua, licha ya kwamba bado kumekuweko mashambulio ya hapa na pale.

Shirika la Haki za Binadamu la Human Rights Watch limearifu kuwa wakaazi wa mji huo wa Osh wanahitaji misaada na kulindwa dhidi ya mashambulio hayo.

Marekani na Urusi zimekuwa na wasiwasi kuwa kuendelea kwa machafuko nchini Kyrgystan, nchi ambayo ni njia ya biashara haramu ya madawa ya kulevya kutokea Afghanistan, kutaweza kusababisha kuzidi wapiganaji wenye misimamo mikali katika eneo hilo la Asia ya kati.

Kwa upande wake, msaidizi wa Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani, Robert Blake, baada ya kutembelea makambi ya wakimbizi yaliyoko katika nchi jirani ya Uzbekistan, ameielezea hali ilivyo katika eneo la kusini mwa Kyrgyzstan kama ni janga la kibinadamu.

Nalo shirika la Afya la Umoja wa Mataifa -WHO- limesema leo kwamba machafuko hayo yaliyotokea Kyrgyzstan yanaweza kuathiri takriban watu milioni moja, huku laki tatu kati yao kuwa wakimbizi.

Mwandishi: Halima Nyanza(reuters, afp)   

Mhariri: Miraji Othman

 • Tarehe 18.06.2010
 • Mwandishi Halima Nyanza
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/NwAe
 • Tarehe 18.06.2010
 • Mwandishi Halima Nyanza
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/NwAe
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com