Hali bado tete Cote d′Ivoire | Matukio ya Kisiasa | DW | 09.03.2011
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Hali bado tete Cote d'Ivoire

Wakati viongozi wa Umoja wa Afrika wakikutana leo kuujadili mzozo wa kisiasa nchini Ivory Coast, hali nchini humo bado ni tete, baada ya majeshi ya serikali kuwaua watu wanne.

default

Mji wa Abidjan, unaokabiliwa na machafuko

Milio ya risasi ilisikika katika maeneo kadhaa ambayo yalifanyika maandamano yaliyowahusisha maelfu ya wanawake, kumtaka Rais Laurent Gbagbo ajiuzulu.

Watu walioshuhudia tukio hilo wamesema wanajeshi wanaomuunga mkono bwana Gbagbo, na kuwaua vijana watatu wa kiume na wa kike mmoja mwenye umri wa miaka 21.

Maandamano hayo yaliyoanza kwa amani yalikuwa yakilindwa na vijana waliobeba silaha, wanaomuunga mkono Ouattara, lakini mara ghafla wakati yakikaribia kumalizika kulisikika milio ya risasi, hali ambayo watu walioshuhudia tukio hilo wanasema inaonesha kuwa kama kulitokea mapigano kati ya makundi mawili.

Tukio hilo limetokea ikiwa ni wiki moja tu, baada ya majeshi yanayoongozwa na Gbagbo kuwaua kwa risasi wanawake saba katika maandamano mengine ya wanawake yaliyofanyika katika mji wa Abobo, mji ambao unamuunga mkono mpinzani wa bwana Gbagbo, Alassane Ouattara.

Kitongoji hicho cha Abobo kwa kiasi kikubwa sasa kinadhibitiwa na wapiganaji wanaomuunga mkono Ouattara, baada ya wiki nzima ya mapigano yaliyowarudisha nyuma pilisi na wanajeshi katika eneo hilo.

Mapigano kati ya wafuasi wa pande hizo mbili yamesababisha kuzorota kwa hali ya usalama katika mji mkuu wa nchi hiyo, Abidjan.

Leo Umoja wa Afrika unakutana mjini Addis Ababa Ethiopia, kuujadili mzozo huo wa kisiasa nchini Cote d'Ivoire.

Alassane Ouattara ambaye anaungwa mkono na jumuia ya kimataifa kesho anatarajia kuhudhuria mkutano huo, licha ya kuwa amewekewa vizuizi na majeshi ya nchi hiyo katika hoteli anayoishi mjini Abidjan.

Hata hivyo Rais Gbagbo binafsi hatarajiwi kuhudhuria mkutano huo na badala yake atatuma wawakilishi wake

Vikwazo vilivyowekwa na jumuia ya kimataifa na juhudi za usuluhishi zilizokuwa zikifanywa na Umoja wa Afrika zimeshindwa kumuondoa bwana Gbagbo madarakani, ambaye Jumatatu ya wiki hii alisema kuwa anachukua udhibiti wa sekta ya zao la taifa, Cocoa.

Mataifa ya magharibi yamemuonya bwana Gbagbo huenda akachunguzwa kwa tuhuma za uhalifu, kwa kushambulia waandamanaji, licha ya kwamba wanajeshi wake wakisema kuwa wanapaswa kufanya hivyo ili kuzuia ghasia za waandamanaji.

Mashirika ya misaada ya Umoja wa mataifa yanaripoti kuwa takriban watu 450,000 wameyakimbia makaazi yao, ikiwemo 90,000 ambao wamekimbilia nchi jirani ya Liberia.

Mwandishi: Halima Nyanza

Mhariri:Abdul-Rahman,Mohammed

 • Tarehe 09.03.2011
 • Mwandishi Halima Nyanza
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/10Vnt
 • Tarehe 09.03.2011
 • Mwandishi Halima Nyanza
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/10Vnt
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com