Hali bado tete Côte d′Ivoire. | Matukio ya Kisiasa | DW | 03.12.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Hali bado tete Côte d'Ivoire.

Côte d'Ivoire imefunga mipaka yote, baada ya Baraza la taifa la katiba, kupinga matokeo yaliyompa ushindi kiongozi wa upinzani Alassane Outtara, kufuatia duru ya pili ya uchaguzi mkuu nchini humo.

default

Kiongozi wa upinzani Alassane Ouattara, ambaye ushindi wake unapingwa na mpinzani wake Laurent Gbagbo.

Akitoa taarifa hiyo katika televisheni ya taifa, Msemaji wa Jeshi la nchi hiyo Meja Kanali Babri Gohourou amesema mipaka yote ya nchi kavu, bahari na anga imefungwa.

Hata hivyo hakutoa sababu za uamuzi huo uliofikiwa.

Kufuatia uamuzi huo uliotolewa na jeshi, chombo cha taifa cha kusimamia vyombo vya habari nchini humo baadaye kilitangaza kuzuia mawasiliano ya televisheni za kigeni pamoja na radio.

Hatua hiyo imekuja baada ya Tume ya uchaguzi nchini humo kumtangaza Ouattara kuwa mshindi wa duru ya pili ya uchaguzi iliyofanyika siku ya Jumapili ambayo ulitawaliwa na vurugu, baada ya kupata asilimia  54 ya kura zote zilizopigwa dhidi ya mpinzani wake, Rais anayetetea kiti chake Laurent Gbagbo aliyepata asilimia 46 ya kura.

Hata hivyo, Mkuu wa baraza la taifa la Katiba Paul Yao N'dre, ambaye ni msirika wa bwana Gbagbo, amesema tangu tume hiyo ya uchaguzi iliposhindwa kutangaza matokeo katika siku ya mwisho iliyowekwa Jumatano ya wiki hii, haikuwa na haki ya kutangaza mshindi.

Kwa sasa baraza hilo linachunguza matokeo ya uchaguzi huo katika majimbo kadhaa, yaliyo ngome ya bwana Outtara, ambayo Bwana Gbagbo ametaka yabatilishwe, kutokana na kile alichodai kwamba ni kitisho na kudhalilishwa kwa wafuasi wake.

Kufuatia hali kutokuwa shwari nchini humo, Ufaransa na Marekani zimewataka wapinzani hao katika kinyang'anyiro cha kuwania Urais nchini  Côte d'Ivoire Alassane Ouattara na Laurent Gbagbo kukubali matokeo ya uchaguzi huo, ambao mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini humo amesema ulikuwa ni wa kidemokrasia.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeonya pia kuchukua hatua dhidi ya yeyote yule atakayejaribu kupinga mchakato huo wa uchaguzi.

Kuchelewa kutangazwa kwa matokeo na tuhuma za udanganyifu zimesababisha kuongezeka kwa hali ya wasiwasi katika nchi hiyo iliyoko Afrika magharibi, ambako watu zaidi ya 10 waliuawa katika ghasia zilizotokea kutokana na duru hiyo ya pili ya uchaguzi.

Ulinzi wa jeshi umeimarishwa katika maeneo kuzunguuka mji mkuu wa nchi hiyo Abidjan, huku Rais Gbagbo ambaye anatetea nafasi yake akiongeza muda wa amri ya kutotembea usiku, mpaka Jumapili.

Aidha jeshi nchini humo lilikiri siku ya Jumatano kuwaua watu wanne katika moja ya ofisi za Bwana Ouattara kaskazini mwa mji mkuu wa nchi hiyo Abidjan.

Rais Gbagbo anayetetea kiti chake na mpinzani wake Bwana Ouattara waziri mkuu wa zamani na aliyekuwa afisa mwandamizi katika shirika la fedha kimataifa IMF, wamepambana katika uchaguzi huo wenye lengo la kumaliza mzimu wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya mwaka 2002, ambao vimegawa waislamu wengi walioko katika kaskazini na wakristo walioko katika eneo la kusini.

Mwandishi: Halima Nyanza(dpa, afp)

Mhariri: Abndul-rahman

 • Tarehe 03.12.2010
 • Mwandishi Halima Nyanza
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/QOkL
 • Tarehe 03.12.2010
 • Mwandishi Halima Nyanza
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/QOkL
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com