1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hakuna usawa wa habari baina ya mataifa tajiri na masikini

Mohammed Khelef
21 Juni 2022

Imebainika kuwa miaka 40 tangu Umoja wa Mataifa kuazimia kuleta usawa wa habari na mawasiliano kati ya mataifa tajiri na masikini, bado pengo baina ya pande hizo ni kubwa sana na kila kukicha linaelekea kutokuzibika.

https://p.dw.com/p/4Czgi
GMF 2022 | Plenary Chamber
Picha: Ronka Oberhammer/DW

Mada iliyozuwa mjadala mzito asubuhi ya Jumanne (Juni 21) kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano mjini Bonn ni ile iliyotaka kujuwa jinsi vyombo vya habari vya ulimwengu uliondelea vinavyoripoti mataifa ya Dunia ya Tatu, ambapo takribani wachokoza mada na wachangiaji wote walinyoosha vidole vyao vya lawama kwa jinsi upotoshaji mkubwa unavyofanyika kwenye eneo hili.

Barkha Dutt, mwandishi wa habari kutoka India anayeandikia pia magazeti mashuhuri ya New York Times na Washington Post ya Marekani, alisema tatizo kubwa lipo kwenye nani mwenye nguvu na nani hana.

"Tatizo la vipi mataifa ya magharibi yanayaangalia mataifa yetu ya ulimwengu wa tatu lina mizizi yake kwenye mtazamo kwamba wanapotuangalia sisi wanatumia kiyoo cha majanga, mambo machafu, mambo magumu. Kama kwamba sisi si watu wa kawaida wenye kuishi maisha ya kawaida. Natuwe wawazi kwamba hili halihusiani na uandishi wa habari pekee, bali linahusu nchi zenye nguvu na madaraka na zinatumia nguvu na madaraka hayo kupotosha mambo," alisema mwandishi wa habari huyo ambaye pia ni muanzilishi wa kampuni ya Butt Media Pvt. Ltd.

Uwekezaji mkubwa wa Magharibi kwenye habari

GMF 2022 | Impressions
Picha: Ronka Oberhammer/DW

Lakini kile kinachoyafanya mataifa ya Magharibi kuwa na nguvu hizo, kwa mujibu wa Tom Oladipo, mwandishi wa habari wa Nigeria, ni kuwa yamewekeza sana kwenye vyombo vyake vya habari na kuvigeuza vyombo hivyo kuwa na uwezo unaovuuka mipaka ya mataifa yao.

"Vyombo vya habari vya kimagharibi ni vikubwa zaidi: vinafika mbali zaidi na vinaathiri jinsi ulimwengu mmoja unavyouangalia ulimwengu mwengine. Mara nyingi watu wanapotaka kuthibitisha kitu, hukitafuta kwenye Google au hufunguwa mitandao ya vyombo vya habari kama BBC, the Guardian ama chochote kile, na baadhi ya wakati hata hawajipi tabu ya kusoma makala nzima, bali husoma tu vichwa vya habari vilivyoandikwa na vyombo hivyo na kisha kutoa hukumu yao," alisema Oladipo, ambaye pia anafanya kazi na shirika la utangazaji la kimataifa la Ujerumani, Deutsche Welle.

Uwasilishaji mbaya wa Afrika

GMF 2022 | Peter Limbourg und Jodie Ginsberg
Picha: Ronka Oberhammer/DW

Pale inapotokea kuwa vichwa hivyo vya habari vimeandika mambo mabaya tu kuhusu ulimwengu wa tatu, mambo hayo mabaya yanakuwa ndiyo tafsiri pekee waliyonayo watu wa mataifa tajiri na hata wale wa mataifa masikini ambao wanaufahamu ulimwengu kupitia vyombo vya habari vya kimagharibi pekee.

Huo ndio ujumbe anaoupata mwandishi wa habari wa shirika la utangazaji la Kenya, KBC, Clare Wanja, ambaye aliiambia DW kwamba kuna mambo mengi yasiyo sahihi yanayoripotiwa kuhusu Afrika.

"Watu huku Magharibi wanadhani kuwa Afrika ni nchi moja kubwa. Tunawaambia hapana, Afrika ina nchi nyingi mno kiasi cha kwamba unaposema Afrika inafanya jambo fulani, tutakuuliza unakusudia nini, wakati hiyo ni nchi moja tu ya Afrika?" Alihoji Wanja ambaye alikuwa pia anahudhuria kongamano.

Wakati kongamano la 15 la kimataifa la vyombo vya habari (GMF)likimalizika kwenye ukumbi wa kimataifa wa mikutano mjini Bonn, ilikuwa wazi kuwa miongo minne ya Umoja wa Mataifa kupitia shirika lake la Sayansi, Utamaduni na Elimu (UNESCO) kuamua kuwa na mfumo mpya wa haki wa habari na mawasiliano ulimwenguni (NWICO) umeshindwa.