1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Haaland yuko fiti kuivaa Bielefeld

11 Machi 2022

Erling Haaland yuko fiti kuichezea klabu yake ya Borussia Dortmund wikendi hii japo huenda akasubiri zaidi kuingia uwanjani kwa sababu ya mlipuko wa ugonjwa wa Covid-19 katika kambi ya wapinzani wao Arminia Bielefeld.

https://p.dw.com/p/48N76
Deutschland Bundesliga | TSG 1899 Hoffenheim vs Borussia Dortmund | Tor (0:1)
Picha: Uwe Anspach/dpa /picture-alliance

Mechi ya Dortmund na Mainz wiki iliyopita ilikuwa ya kwanza ya Bundesliga msimu huu kuahirishwa kutokana na maambukizo ya virusi vya Corona.

Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari ambazo bado hazijathibitishwa zinasema huenda mechi ya Jumapili hii kati ya Dortmund na Bielefeld ikaahirishwa.

Kocha wa Dortmund Marco Rose amesema, "Ndio, janga la Covid-19 limekuwa kero kwa kila mtu. Tunaomba kila kitu kirudi kama kawaida. Tumejiandaa sawa kwa ajili ya mchezo."

Haaland anarudi uwanjani baada ya jeraha la msuli wa nyuma ya paja kumuweka nje kwa muda mrefu.

Kocha Marco Rose hata hivyo atazikosa huduma za Mats Hummels, Raphael Guerreiro, Manuel Akanji, Dan-Axel Zagadou, Thomas Meunier, Mateu Morey, Marco Reus, Youssoufa Moukoko na Steffen Tigges.

Rose amefichua kuwa mshambualiji kinda raia wa Marekani Giovanni Reyna ambaye amekuwa akiandamwa na majeraha msimu huu, pia amerejea mazoezini wiki hii na pia huenda akajumuishwa kikosini wikendi hii.

Dortmund iko katika nafasi ya pili na alama 50, alama tisa nyuma ya mabingwa watetezi Bayern Munich inayoongoza jedwali la Bundesliga kuelekea mechi za wikendi hii.