Guterres kufanya mabadiliko ya kuzuia migogoro | Matukio ya Kisiasa | DW | 11.01.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Guterres kufanya mabadiliko ya kuzuia migogoro

Katibu Mkuu mpya wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, amelitaka Baraza la Usalama la umoja huo, kuchukua hatua zaidi kuzuia migogoro duniani kote huku akiahidi kuimarisha uwezo wa upatanishi wa umoja huo.

Guterres, Waziri Mkuu wa zamani wa Ureno na aliyekuwa mkuu wa shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa, amesema nafasi nyingi za kuzuia migogoro zimepotezwa kwa sababu hakuna uaminifu miongoni mwa mataifa mbalimbali pamoja na kuwepo wasiwasi juu ya uhuru wa nchi zao. Akilihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa mara ya kwanza, tokea aupokee wadhifa huo kutoka kwa Katibu Mkuu aliyemtangulia Ban Ki-moon, Guteress ameahidi kufanya mabadiliko ndani ya Umoja wa Mataifa.

Mwandiplomiasia huyo mwenye umri wa miaka 67, anatarajiwa kujihusisha zaidi katika migogoro inayoendelea duniani kuliko mtangulizi wake, ambaye jitihada za upatanishi aliwaachia zaidi wajumbe wake maalum.

"Kinga lazima iwe kipaumbele chetu cha kawaida. Ukweli ni kwamba, tukizuia migogoro kutokea tunaweza kuepuka na mateso. Tukiepusha migogoro tutaepukana na uharibifu. Ni vyema zaidi kuzuia mgogoro, kuliko kuitikia,” amesema Antonio Guterres.

New York UN Generalsekretär Antonio Guterres (Reuters/S. Keith)

Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa

Baraza hilo la Umoja wa Mataifa, kwa kiasi kikubwa limekosa maafikiano juu ya vita ya miaka sita vya Syria vilivyosababisha vifo vya zaidi ya watu 310,000, wakati Urusi na China wakiendelea kupingana na Marekani, Uingereza na Ufaransa kuhusu mgogoro huo wa Syria.

Umoja huo pia umegawanyika juu ya mbinu nyingine za kutumia katika migogoro na majanga kama vile ya Sudan Kusini na Burundi, na baadhi ya washirika wakitoa sababu ya kuwa na wasiwasi juu ya uhuru wa nchi zao.

Guterres amelitaka Baraza la Usalama kutumia kifungu cha sita cha mkataba wa Umoja wa Mataifa, ambacho kinauruhusu umoja huo kufanya uchunguzi na kupendekeza taratibu za kutatua migogoro, ambayo hatimaye inaweza kuhatarisha amani na usalama.

Kiongozi huyo wa Umoja wa Mataifa, aliainisha hatua anazozichukua kuimarisha uwezo wa Umoja wa Mataifa wa kuzuia migogoro, na kusema kuwa umoja huo umegawanyika kwa sasa. Ameunda kamati ya utendaji, itakayokuwa na kazi ya kuviunganisha vikosi vyote vya umoja huo. Pia ameteua afisa mwandamizi, atakayechanganisha uwezo wa Umoja wa Mataifa wa kuzuia migogoro ili kupatikane hatua imara zaidi.

Baaade wiki hii, Guteress atafanya ziara yake ya kwanza kama Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Ataelekea mjini Geneva, Uswisi kushuhudia mazungumzo ya amani kuhusu kisiwa cha Cyprus kilichogawanyika kati ya upande wa Ugiriki na Uturuki. Na, atarudi tena Geneva wiki inayofuata kukutana na Rais wa China, Xi Jinping, ambaye ushirikiano wake na Umoja wa Mataifa umekuwa ukiongezeka siku za karibu.

Mwandshi: Yusra Buwayhid/afp/rtre

Mhariri: Grace Patricia Kabogo

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com