1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Guterres asikitishwa na kiwango cha fedha kuisaidia Yemen

2 Machi 2021

Antonio Guterres ameonya juu ya kile alichokitaja kama "hukumu ya kifo kwa familia za Yemen" baada ya mkutano wa wafadhili wa kimataifa kupata chini ya nusu ya fedha zinazohitajika ili kuzuia baa la njaa nchini humo.

https://p.dw.com/p/3q5A9
UN-Generalsekretär  Antonio Guterres
Picha: picture-alliance/ Pacific Press/L. Radin

Mkutano huo wa wafadhali wa kimataifa ulifanikiwa kupata dola bilioni 1.7 pekee. Guterres ameonyesha kusikitishwa na kiwango hicho cha fedha.

Katika mkutano uliofanyika kwa njia ya Video, katibu mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa alikuwa anakusudia kuchangisha angalau dola bilioni 3.85 mwaka huu ili kushughulikia mahitaji ya watu nchini Yemen wanaokabiliwa na baa la njaa.

Hata hivyo, fedha za mwaka huu zilikuwa kidogo tofauti na fedha ambazo Umoja wa Mataifa ulipata mwaka uliopita.

Vile vile, fedha hizo zilikuwa pungufu ya dola bilioni moja tofauti na kiwango cha fedha kilichoahidiwa katika mkutano wa mwaka 2019.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya uratibu wa masuala ya kibinadamu imeonya kuwa zaidi ya watu milioni 16 watakabiliwa na njaa mwaka huu, huku tayari nusu kati yao wakiishi katika mazingira magumu ya ukosefu wa lishe bora.

Watoto milioni 2.3 wana utapiamlo

Weltspiegel 17.02.2021 | Jemen Krieg | Mädchen in Flüchtlingslager
Picha: Nabeel al-Awzari/REUTERS

Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amewatolea wito viongozi duniani kufikiria tena jinsi wanavyoweza kusaidia ili kuzuia baa la njaa.

"Leo, kupunguza misaada ya fedha ni kama hukumu ya kifo kwa familia. Wakati vita vikiendelea, watoto wa Yemen ndio wanaoathirika zaidi."

Yamkini kuanzia mwanzo ilikuwa dhahiri kuwa wafadhali hawangeweza kuchangisha dola bilioni 3.85 kutokana na athari za kiuchumi zilizosababishwa na janga la virusi vya Corona. Juu ya hayo, madai ya ufisadi katika shughuli za misaada nchini Yemen pia zimechangia kwa mchango huo kupungua.

Vita vya Yemen vilianza mnamo mwaka 2014 baada ya waasi wa Kihouthi wanaoungwa mkono na Iran kuchukua udhibiti wa mji mkuu wa Sanaa na sehemu kubwa ya eneo la kaskazini mwa nchi hiyo.

Mzozo nchini Yemen umesababisha vifo vya watu wapatao 130,000 na kuitumbukiza nchi hiyo katika janga baya zaidi la kibinadamu. Nusu ya vituo vya afya vimefungwa au kuharibiwa huku Wayemen milioni 4 wakikimbia makwao.

Rekodi zinaonyesha kuwa watoto milioni 2.3 wana utapiamlo na takriban watoto 400,000 wenye chini ya umri wa miaka mitano wanakabiliwa na kifo iwapo hawatopata haraka msaada wa chakula.