Gladbach iko tayari kukwaruzana na Bayern | Michezo | DW | 24.10.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Gladbach iko tayari kukwaruzana na Bayern

Viongozi wa ligi Bayern wanashuka dimbani katika mtihani wao mkali kabisa wa msimu huu watakapocheza ugenini Jumapili dhidi ya nambari mbili Borussia Mönchengladbach.

Timu zote mbili hazijashindwa mchuano hata mmoja katika Bundesliga msimu huu, huku bayern wakiwa kileleni na pengo la points nne. Lucien Favre ni kocha wa Gladbach na anasema vijana wake wanajiandaa kushuka dimbani bila hofu "bila shaka tunawaheshimu sana Bayern lakini hatuwaogopi. Tuna hofu kidogo ambayo ni muhimu katika kuwa makini, pamoja na maandalizi. Tunajua uwezo wao. Tumeona mechi yao mwisho waliyowafunga Roma mabao saba kwa moja ugenini. Roma ni timu kubwa Italia na hilo linaelezea kila kitu. Ilikuwa kazi rahisi wka Bayern. Walicheza kandanda safi na hilo linaonekana wazi na tunakubali. Lakini tunajiandaa na tutaona itakavyokuwa".

Bayern bado hawana huduma za wachezaji Bastian Schweinsteiger, Holger Badstuber na Thiago Alcantara ambao wanauguza majeraha lakini kikosi chao bado kinaonekana kuwa imara na tayari kuendeleza mchezo wao mzuri. Bayern wameshinda mechi tatu za mwisho dhidi ya Gladbach lakini rekodi yao ya Bundesliga katika uwanja wa Borussia Park ni mbovu, kwa sababu wamewahi kushinda mechi 11 pekee kati ya 46.

Mpambano mwingine wa Jumapili ni vita kati ya nambari tano na nne kwenye ligi wakati Wolfsburg ikiialika Mainz, nayo nambari tatu Hoffenheim ikilenga kuendeleza matokeo yao mazuri nyumbani kwa kuialika Paderborn, ambao katika nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi.

Vilabu vingine viwili vya Ujerumani vinavyocheza katika Champions League, Bayer Leverkusen na Schalke, vinakutana katika mchuano wa baadaye leo usiku vikilenga kuimarisha nafasi zao kwenye ligi. Leverkusen kwa sasa iko katika nafasi ya sita wakati Schalke ikipambana katika nafasi ya tisa.

Katika upande wa mkia wa msimamo wa ligi, nambari mbili kutoka nyuma Freiburg ambayo haijashinda mchuano hata mmoja msimu huu, itasafiri kuchuana ugenini dhidi ya Augsburg, wakati SV Hamburg ambao iko katika nafasi ya 16 ikipambana na Hertha Berlin. Makamu bingwa wa msimu uliopita Borussia Dprtmund wanataraji kuanzisha harakati za kupanda juu ya msimamo, kutoka nafasi ya 14, kwa kucheza nyumbani dhidi ya Hanover wakati Eintracht Frankfurt ikipambana nyumbani na Stuttgart.

Mwandishi: Bruce Amani/DPA
Mhariri: Yusuf Saumu