Ghana yashinda | Michezo | DW | 21.01.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Michezo

Ghana yashinda

Michuano ya fainali za 26 za kombe la mataifa ya Afrika zimeanza jana huko Ghana ambapo wenyeji wameanza vyema michuano hiyo. Ghana ilifanikiwa kuifunga Guinea mabao 2-1 kati mechi ya ufunguzi jana usiku jijini Accra

default

John Pantsil wa Ghana kushoto na Kanfory Sylla Guinea wakiwania mpira katika mechi ya ufunguzi wa kombe la mataifa ya afrika jana mjini Accra. Ghana ilishinda kwa mabao match 2-1.

Bao la dakika za majeruhi lililopachikwa kiufundi na Sulley Muntari lilishusha pumzi za waghana na kuwafanya kuianza vyema michuano hiyo kwa ushindi huo.


Mapema Asamoh Gyan aliitanguliza mbele Ghana kwa bao la mkwaju wa penalti, kabla ya Oumar Kalabane kuisawazishia Guinea.


Ikionekana kana kwamba mpambano huo utamalizika kwa sare, ghafla, Sulley Muntari anayechezea Portsmouth ya Uingereza akiwa kiasi cha mita 25 alivurumisha kombora lililokwenda moja kwa moja wavuni na kuamsha shangwe na nderemo.


Winga wa kulia wa Ghana Laryea Kingsotn alisema hali ya hewa ya kwao ni changamoto kubwa.


Lakini kocha wa timu hiyo ya Ghana Claude Le Roy, alilalamikia hali mbaya ya dimba akisema imewazuia vijana wake kutandaza soka la kuvutia.


Amesema kuwa katika uzoefu aliyonao wa miaka 20 wa kufundisha soka barani afrika hajawai kukumbana na dimba bovu kama la uwanja wa Ohene Djan.


Kwa upande wake kocha wa Guinea Robert Nouzerat alisema timu yake ilicheza chini ya kiwango inachostahili kucheza.


Kabla ya mechi hiyo, waumini wa dini ya kikristo nchini Ghana walimiminika makanisani huku wakiwa na nguo za bendera ya nchi hiyo, ambapo kuliendeshwa ibada maalum za kuiombea ushindi.


Imani za kishirikina maarufu kama juju nazo hazikuwekwa nyuma.


Kundi moja la washabiki lilibeba chungu kilichokuwa kikichemka juju, ambapo mmoja wao Kojo Saaka alisema juju hiyo inafukuza mashetani dimbani na kufungua njia kwa ghana kushinda.


Michuano hiyo inaendelea leo kwa mechi tatu, ambapo Mali itaingiliana na Benin katika kundi B ambapo katika A Namibia itacheza na Morocco.


Lakini ni mechi nyingine ya kundi B kati ya tembo wa Ivory Coast na Tai wa kijani wa Nigeria inayosubiriwa kwa hamu kubwa.


Pambano hilo litawakutanisha wachezaji wawili wa Chelsea ya Uingereza, Didier Drogba wa Ivory Coast na chipukizi Obi Mikel wa Nigeria.


 • Tarehe 21.01.2008
 • Mwandishi Liongo, Aboubakary Jumaa
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CvDZ
 • Tarehe 21.01.2008
 • Mwandishi Liongo, Aboubakary Jumaa
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CvDZ