1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ggabgo kurejea nyumbani baada ya takriban muongo mmoja

John Juma
17 Juni 2021

Rais wa zamani wa Ivory Coast Laurent Gbagbo, anarejea nchini mwake Alhamisi kwa mara ya kwanza katika kipindi cha takriban muongo mmoja.

https://p.dw.com/p/3v58s
Niederlande Den Haag I Prozess Elfenbeinküste am Internationalen Gerichtshof
Picha: Jerry Lampen/AP/picture alliance

Hii ni baada ya mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC kumfutia mashtaka ya uhalifu dhidi ya ubinadamu. 

Gbagbo anarejea baada ya aliyekuwa hasimu wake mkubwa kisiasa na rais wa sasa kumkaribisha nyumbani katika misingi ya maridhiano.

Gbagbo anatarajiwa kuwasili katika mji mkuu wa Ivory Coast Abidjan, mwendo wa saa kumi kasorobo majira ya Afrika magharibi, akitokea Brussels Ubelgiji.

Amekuwa akiishi Brussels tangu mahakama ya kimataifa ICC ilipofuta mashtaka dhidi yake na kumuachilia huru mwaka 2019. Rufaa dhidi ya uamuzi huo ulioshangaza pia ilishindwa mnamo mwezi Machi mwaka huu, hivyo kumsafishia njia ya kurudi nyumbani.

Mahakama ya kimataifa ya Jinai ICC ilifuta mashtaka dhidi ya Gbagbo.
Mahakama ya kimataifa ya Jinai ICC ilifuta mashtaka dhidi ya Gbagbo.Picha: Peter Dejong/AP/picture alliance

Kurudi nyumbani kwa Gbagbo mwenye umri wa miaka 76, kutakuwa kama mtihani wa udhibiti wa Ivory Coast. Taifa ambalo linaongoza ulimwenguni kote katika uzalishaji wa kakao na pia taifa tajiri zaidi miongoni mwa nchi za Afrika zinazozungumza lugha ya Kifaransa magharibi mwa Afrika.

Aliondoka nchini mwake Ivory Coast mnamo mwaka 2011, baada ya kukataa kukubali kushindwa kwenye uchaguzi uliokumbwa na machafuko. Hatua hiyo ilisababisha kukamatwa kwake na kufunguliwa mashtaka katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC mjini the Hague.

Soma pia: Laurent Gbagbo akana mashtaka ICC

Alipinduliwa madarakani Aprili mwaka 2011, baada ya takriban watu 3,000 kuuawa kwenye machafuko ya kisiasa yaliyodiumu kwa miezi kadhaa kufuatia hatua yake kung'ang'ania madaraka licha ya kushindwa kwenye uchaguzi na rais wa sasa Alassane Ouattara.

Lakini hayo ni ya kale, kwa sasa Gbagbo anaangaziwa kama kiongozi wa kitaifa, anayeitwa kusaidia katika mchakato wa kuleta maridhiano ya kitaifa baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka uliopita ambao pia ulikumbwa na vurugu na kusababisha vifo vya watu kadhaa.

Rais wa Ivory Coast Alassane Ouattara.
Rais wa Ivory Coast Alassane Ouattara.Picha: Yvan Sonh//XinHua/dpa/picture alliance

Rais Ouattara mwenye umri wa miaka 79 ndiye ameongoza mchakato wa kurudi kwa Gbagbo kwa kuhakikisha amepewa pasipoti ya kidiplomasia na kuamuahidi tunu nyinginezo Pamoja na hadhi ya utambulisho kama marais wengine wa zamani.

Rais Ouattara pia ameruhusu Gbagbo kutumia ukumbi wa rais atakapowasili katika uwanja wa ndege mjini Abidjan. Mahema kadhaa yamewekwa kwa watu mashuhuri kumshangilia arejeapo.

Baadaye, atasafiri hadi mtaa wa Attoban ambako makao yake makuu ya kampeni ya mwaka 2010 yako. Hayo ni kulingana na chama chake cha Ivorian Popular Front (FPI)

Wafuasi wa Gbagbo wakiwa na bango lenye picha yake katika mji wa Gagnoa Juni 13, 2021.
Wafuasi wa Gbagbo wakiwa na bango lenye picha yake katika mji wa Gagnoa Juni 13, 2021.Picha: SIA KAMBOU/AFP/ Getty Images

Msafara wa Gbagbo utapitia maeneo kadhaa ambako wafuasi wake wanatarajiwa kukusanyika kumshangilia na kumkaribisha.

Chama chake kimekuwa kikiwasiliana na serikali kuhusu mipango ya sherehe, lakini serikali imependelea sherehe ya watu wachache.

Hata hivyo msemaji wa Gbagbo ameliambia shirika la Habari la AFP kwamba hakuna maagizo kutoka kwa serikali kuzuia mikusanyiko.

Tayari sherehe zimeshaanza mjini Abidjan wakisubiri kurudi kwake.     

Katika jimbo la Gagnoa ambako ndiko anatokea na ambako ni ngome yake kuu, picha yake imechorwa kwenye nguo na kofia ambazo wafuasi wake wamevaa, wakisema Simba wa Afrika amerudi.

(AFP)