Gaddafi bado ngangari | Matukio ya Kisiasa | DW | 26.04.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Gaddafi bado ngangari

Licha ya maroketi ya Jumuiya ya Kujihami ya NATO dhidi ya makaazi yake, kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi, bado anaonekana imara, huku waasi mjini Misrata wakifanikiwa kuwarudisha nyuma wanajeshi wa kiongozi huyo.

Kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi

Kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi

"Kiongozi wetu anafanya kazi zake salama usalimini, akiwa mjini Tripoli. Yu mzima bukheri wa afya na anaongoza vita hivi kwa maslahi ya amani na demokrasia". Ndivyo msemaji wa Gaddafi, Musa Ibrahim, alivyowaambia waandishi wa habari, katika mkutano uliohudhuriwa pia na maafisa kadhaa wa kibalozi.

Kauli hii ya serikali ya Libya inakuja kufuatia mashambulizi ya hapo Jumatatu (25.04.2011) yaliyofanywa na vikosi vya NATO katika makaazi ya Gaddafi na kuliharibu kabisa jengo ambalo NATO inadai kilikuwa kituo cha mawasiliano ya kuendeshea vita kwa upande wa utawala wa Gaddafi.

Hata hivyo, serikali ya Libya inasema kwamba mashambulizi hayo yalikusudiwa kumuua kiongozi huyo, lakini yakamkosa na badala yake kuuwa watu wengine watatu na kujeruhi 45.

Waasi wawarudisha nyuma wanajeshi wa Gaddafi

Ndege inayojiendesha yenyewe ya Marekani kwenye operesheni ya NATO

Ndege inayojiendesha yenyewe ya Marekani kwenye operesheni ya NATO

Kwengineko, katika mji ulio mashariki ya Tripoli wa Misrata, waasi wanasema kwamba wamefanikiwa kuwaondoa wanajeshi wa Gaddafi waliokuwa wameuzingira mji huo kwa wiki saba sasa.

Lakini madai haya ya ushindi yanatiliwa shaka na kuendelea kwa makombora yanayovurumishwa mjini humo kutokea upande wa vikosi vya Gaddafi.

Mpiganaji mmoja wa waasi ameliambia Shirika la Habari la AFP kwamba upo uwezekano wa baadhi ya wanajeshi mmoja mmoja wa Gaddafi kubakia ndani ya mji walikojificha kwa khofu ya kuuawa, lakini hakuna makundi makubwa ya wanajeshi hao.

Maafa ni makubwa

Seneta John McCain wa Marekani akizungumza na waandishi wa habari mjini Benghazi Aprili 22, 2011.

Seneta John McCain wa Marekani akizungumza na waandishi wa habari mjini Benghazi Aprili 22, 2011.

Hata hivyo, taarifa kutoka hospitali ya Mujamaa Tibi zinasema kwamba maafa kwa upande wa raia yamekuwa ni makubwa, licha ya ushindi huu unaotajwa na waasi. Majeruhi na maiti kadhaa zimeonekana zikipelekwa kwenye hospitali hiyo.

Mmoja wa madaktari wa Misrata, Mohammed Al-Fajieh, anasema kwamba, nyingi ya majeruhi na maiti hizo zimeungua kabisa, jambo ambalo linaifanya kazi yao kuwa ngumu sana:

"Ni vigumu kwetu kuwatibu watu sasa. Kwa hakika, nyoyo zetu zimevunjika. Baadhi ya wakati mimi na madaktari wenzangu hutamani kulia." Amesema Dk. Al-Fajieh.

Kwa mujibu wa taarifa za kitabibu, mashambulizi ya jana peke yake kwenye mji wa Misrata yamegharimu maisha ya watu wasiopungua darizeni moja na wengine 20 kujeruhiwa, huku wengi wao wakiwa raia wa kawaida, wakiwemo watoto.

Hata hivyo, waasi wameapa kupambana hadi mwisho. Kijana mmoja, ambaye baba yake, ami yake na ami yake ni miongoni mwa waliokufa kwa mashambulizi ya Jumatatu, ameapa kuendelea na mapambano.

"Baba yangu alikuwa na miaka 92. Aliishi na kupigana dhidi ya ukoloni wa Italia. Alishuhudia vita vya kwanza na vya pili vya dunia. Na matarajio yake ilikuwa ni kuuona mwisho wa Gaddafi. Tutaendelea na mapambano hadi tuikomboe nchi yetu kutoka utawala huu wa kikatili." Amesema kijana huyo.

Umoja wa Afrika wakutana na mahasimu wa Libya

Baadhi ya wakimbizi waliokwama nchini Libya

Baadhi ya wakimbizi waliokwama nchini Libya

Katika uwanja wa kimataifa, Umoja wa Afrika umeendelea na jitihada zake za kutafuta suluhu ya amani ya mgogoro huu wa Libya. Hapo Jumatatu, ujumbe wa Umoja huo ulifanya mazungumzo kwa nyakati tafauti na waziri wa mambo ya nje wa Libya, Abdelati Obeidi, na wawakilishi wa waasi juu ya mpango wa kuacha mapigano.

Mwezi uliopita, upande wa waasi uliukataa mpango wa amani wa Umoja wa Afrika kwa kuwa haukuwa ukijumuisha madai yao ya kuondoka madarakani kwa Gaddafi, huku Marekani, Uingereza na Ufaransa zikisema kwamba hakutakuwa na suluhisho la kisiasa kabla ya Gaddafi kuondoka.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Othman Miraj

DW inapendekeza

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com