FIFA yachelewesha ukaguzi wa viwanja Brazil baada ya mzozo | Michezo | DW | 10.03.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

FIFA yachelewesha ukaguzi wa viwanja Brazil baada ya mzozo

Brazil imesema kuwa mzozo wake na Shirikisho la Soka Ulimwenguni FIFA kuhusu matamshi yenye utata ya Katibu Mkuu ya mwendo wa ukarabati wa viwanja vya michezo umekwisha.

View of construction works at the Mineirao stadium, in preparation for the FIFA 2014 World Cup, in Belo Horizonte, Minas Gerais state, in Brazil, on Friday, August 26, 2011. Photo: CRISTIANO COUTO/JORNAL HOJE EM DIA/AE

Brasilien Fußball WM 2014 Mineirao Stadion

Hata hivyo FIFA imesema kuwa Katibu Mkuu wake Jerome Valcke ameahirisha ziara yake nchini Brazil. Waziri wa Michezo wa Brazil Aldo Robelo aliwaambia waandishi wa habari kuwa suala hilo limekwisha. Aliyasema hayo kabla ya kuukagua uwanja wa kihistoria wa mjini Rio, Maracana ili kuangalia hatua za ukarabati.

Valcke ambaye alizua mjadala mkali wiki iliyopita alipolalamika kuwa waandalizi hao wa fainali za Kombe la Dunia mwaka 2014 wanahitaji kupigwa teke kwenye makalio kwa sababu ya kuchelewesha maandalizi, alihairisha ziara yake iliyotarajiwa kuanza Jumatatu.

FIFA mapema wiki hii iliomba radhi kutokana na matamshi hayo ya Valcke, ambayo yaliyakasirisha mamlaka ya Brazil. Taarifa ya FIFA imesema ziara hiyo ya Valcke kukagua kazi ya ujenzi wa Recife, Brasilia na Cuiaba, viwanja vitatu kati ya 12 vitakavyotumiwa na Brazil katika mechi za Kombe la Dunia, itapangwa upya baada ya mkutano uliopangwa na Rais wa Brazil Dilma Rousseff na mwenzake wa FIFA Sepp Blatter.

Podolski njiani kuelekea Arsenal

FC Cologne na Arsenal bado zimenyamaza kimya kuhusu madai ya uhamisho wa Lukas Podolski

FC Cologne na Arsenal bado zimenyamaza kimya kuhusu madai ya uhamisho wa Lukas Podolski

Mshambuliaji wa Ujerumani Lukas Podolski ataihama klabu yake ya FC Cologne mwishoni mwa msimu ili kujiunga na Arsenal kwa kima cha euro milioni 13. klabu hiyo ya Ujerumani ambayo iko katika nafasi ya 14 kwenye Bundesliga, haijadhibitisha madai hayo lakini gazeti la Ujerumani Bild , limesema Podolski amekubali kanuni za mkataba na kmalbu hiyo ya Premier League ya Uingereza. Gazeti la Express la mjini Cologne limedai kile kinachokosekana tu ni sahihi ya mchezaji huyo kwenye mkataba wa Arsenal. Gazeti la Bild linadai Podolski amekubali masharti ya mkataba huo wa miaka minne.

Kocha wa timu ya soka ya Ujerumani Joachim Loew amekanusha uvumi unaomhusisha na kazi ya ukufunzi wa klabu ya Uingereza Chelsea. Loew amesema lengo lake kwa saa ni katika dimba lijalo la EURO 2012. Loew amesema kwa sasa anachokifiri tu ni wachezaji wake, na kuziangalia timu nyingine katika maandalizi ya dimba hilo la Ulaya litakaloanza katika miezi mitatu ijayo.

Bado mimi ni wa Bayern: kocha Heynckes

Mkufunzi wa Bayern Munich Juppe Heynckes amesema ananuia kuendelea kuiongoza klabu hiyo ya ligi ya Bundesliga huku akiwa amesalia na miezi 15 mkataba wake ukikamilika, licha ya ripoti za vyombo vya habari kudai kuwa anataraji kujizulu mwishoni mwa msimu.

Jupp Heynckes anakummbwa na shinikizo katika klabu ya Bayern

Jupp Heynckes anakummbwa na shinikizo katika klabu ya Bayern

Bayern ilisema wiki hii kuwa wanatathmini hatua za kisheria baada ya gazeti moja la Ujerumani The Bild kuripoti kuwa Heynckes ataondoka mwezi Mei. Lakini kocha huyo alisema anazipuuza ripoti hizo, na hazitamwangusha kamwe.

Huku kukiwa kumesalia miezi mwili na mechi kumi kuchezwa msimu huu, nambari mbili Bayern wako alama saba nyuma ya viongozi Borussia Dortmund katika ligi ya Bundesliga. Matumaini ya Heynckes kuimarisha ndoto za Bayern yalipigwa jeki baada ya kurejea mazoezini kiungo Bastian Schweinsteiger aliyekuwa mkekani tangu mwezi Februari kwa sababu ya jeraha.

Mshambuliaji wa klabu ya Hanover 96 Mame Diouf hatacheza kwa wiki kadhaa baada ya kupata jeraha la kifundo cha mguu katika mchuano wao wa Europa League dhidi ya Standard Liege siku ya Alhamisi.

Raia huyo wa Senegal aliyejiunga na klabu hiyo kutoka Manchester United, alipata jeraha hilo katika kipindi cha pili cha mchuano lakini akaendelea na kufunga bao la kusawazisha kabla ya kuondoka uwanjani akichechemea. Hanover walitoka sare ya magoli mawili na Standard Liege.

Mwandishi: Bruce Amani/Reuters/DPA

Mhariri: Abdul-Rahman