1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dola bilioni 1.4 za kimarekani zatengwa kwa ajili ya uokoaji

6 Januari 2020

Australia imesema iko tayari kufanya chochote ili kusaidia watu walioathiriwa na moto nchini humo. Serikali imetenga dola bilioni 1.4 za kimarekani kwa ajili ya juhudi za uokoaji wakati moto huo ukiendelea kuongezeka

https://p.dw.com/p/3Vmr2
BG Waldbrände in Australien | Glut
Picha: AFP/S. Khan

Ahadi ya waziri mkuu Scott Morrison ya kuongeza msaada kwa ajili ya shughuli za uoakoaji inajiri wakati ambapo nchi hiyo imeathirika na moto wa msituni ambao umesababisha vifo vya zaidi ya watu 25 na kuwaacha mamia bila ya makaazi. Waziri mkuu huyo amesema fedha hizo zitatumika kujenga upya miji na miundo mbinu iliyoharibiwa.

Scott Morrison amesema, "Moto bado unawaka, na  utaendelea kuwaka kwa miezi kadhaa ijayo na ndio maana nimetoa kiwango hiki cha pesa dola bilioni 1.4 za kimarekani, lakini iwapo pesa zaidi zitahitajika, zitatolewa pia."

Hata hivyo licha ya tangazo lake la msaada, Morrison amekosolewa vikali na raia wengi wa Australia kwa jinsi anavyolishughulikia janga hilo la moto.

Kundi la kupigania uhifadhi wa mazingira la Green Peace limesema kuwa msaada wa fedha alioutangaza Morrison ni mdogo mno na hautasaidia chochote likiulinganisha na tone katika bahari.

Mkuu wa kampeni wa kundi hilo Jamie Hanson ametaka kampuni za makaa ya mawe na mafuta kuwajibishwa kutoa misaada ya fedha kwani ndizo zinazochangia uchafuzi wa mazingira na kusababisha majanga kama hayo ya moto.

Tayari mwili wa mwanamume wa miaka 71 umepatikana hii leo katika jimbo la New South Wales. Mara ya mwisho kwa mwanamume huyo kuonekana ilikuwa ni mkesha wa mwaka mpya akiwa nyumbani kwake eneo la Pwani ya Kusini. Polisi imesema kuwa imeupata mwili huo karibu na nyumba yake iliyoteketezwa na moto.

Vile vile polisi imeongeza kuwa imewachukulia hatua za kisheria watu 183, wakiwemo mvulana wa miaka 16 kwa makosa yanayohusiana na kuwasha moto kimakusudi.

BG Waldbrände in Australien | Hilflos
Kijana wa kiume akijaribu kuzima moto huko AustraliaPicha: AFP/W. West

Wakati huo huo, hii leo kumeshuhudiwa mvua katika maeneo ya New South Wales na Victoria. Mvua hiyo inaripotiwa kuleta afueni kukabiliana na moto. Gavana wa jimbo la Victoria Daniel Andrews amesema kuwa mvua hiyo imefungua mwanya wa kusafirisha misaada kwa jamii zilioathirika.

Hata hivyo, mamlaka nchini humo zinaonya kuwa mvua hiyo haina uwezo wa kukabiliana na moto huo kwa muda mrefu.

Aidha eneo la New South Wales limeshuhudia mioto ya msituni ipatayo 140 huku eneo la Victoria likishuhudia mioto  39 kama hiyo japo ikisemekana kuwa ya kadri.

Kwa sasa zaidi ya hekari milioni 7 za ardhi imeharibiwa tangu moto huo wa msituni ulipoanza mnamo mwezi Septemba, mwaka uliopita.

DPA/AP/