1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Familia ya mbunge Cherubin DRC yapinga ripoti ya kifo chake

Saleh Mwanamilongo
2 Machi 2024

Familia ya mbunge Cherubin Okende aliyeuwawa nchini Kongo miezi saba iliopita imepinga ripoti ya uchunguzi wa mwendesha mashtaka iliyohitimisha kwamba mwanasiasa huyo w aupinzani alikufa kwa kujitoa muhanga.

https://p.dw.com/p/4d6da
DR Kongo | Cherubin Okende
Mwanamume akiwa amebeba bango la kumbukumbu ya Cherubin Okende, mshirika wa karibu wa Moise Katumbi aliyeuawa Julai 2023 katika mazingira ya kutatanisha, wakati wa mkutano wa uchaguzi wa Katumbi katika uwanja wa michezo mjini Goma, Novemba 23, 2023. Picha: Alexis Huguet/AFP/Getty Images

Akizungumza na waandishi habari mjini Kinshasa, mwendesha Mashtaka Mkuu, Firmin Mvonde, alitangaza kwamba Chérubin Okende alijiua kwa kujipiga risasi.

''Uchunguzi ulihusu matumizi ya risasi, mawasiliano, mwili wa marehemu na madakatari wa upasuaji wa maiti. Na uchunguzi wa maiti unaonyesha Okende alikufa kufuatia na kuvuja damu kutokana na kidonda kilichosababishwa na silaha aliyotumia mwenyewe."

Kauli hii inakuja ikiwa ni sehemu ya kesi inayohusu kifo cha aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, aliyepatikana amefariki kwenye gari lake Julai 13, 2023 huko Kinshasa. Kulingana na hitimisho la uchunguzi, alijiua mwenyewe, kwa kujipiga risasi kwenye kichwa chake.

Ripoti hiyo ya uchunguzi imefuta nadharia kadhaa juu ya tukio hili. Kwanza ripoti ya uchunguzi inaeleza kuwa Okende hakuwepo siku moja kabla ya kifo chake saa kumi alasiri katika Mahakama ya Katiba. Simu yake wakati huo ilionekana katika mtaa mwengine mbali na mahakama ya katiba.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Kinshasa | Cherubin Okende
Cherubin Okende, waziri wa zamani wa uchukuzi na akiwa katika maandamano ya upinzani mjini Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Machi 11, 2023.Picha: Samy Ntumba Shambuyi/AP/picture alliance

Zaidi ya hayo, mwili wake haukuwa umejaa risasi, kama wanavyodai baadhi ya watu. Kulikuwa na risasi moja tu, alisema mwanasheria wa Kongo, na kuthibitisha kwamba lililopigwa kutoka ndani ya gari la Cherubin Okende, ambapo hayati alipatikana akiwa amefariki akiwa peke yake kwenye kiti cha dereva, kulingana na Mwanasheria Mkuu.

Ni mwisho wa miezi mingi ya kusubiri, hasa kwa familia ya hayati Okende, ambayo ilitaka kujua ukweli wa kifo hiki cha kusikitisha. Wakili wa familia ya Okende ameita ripoti hiyo ya mwendesha mshata mkuu wa taifa kuwa ni matusi kwa marehemu Okende na familia yake.

Alexis Dewaef, wakili wa Ubelgiji wa familia ya Okende alikanusha na kutupilia mbali nadharia ya mbunge huyo wa chama cha Moise Katumbi kujiua.

Soma pia: Upinzani Kongo wataka wachunguzi kutoka nje mauaji ya Okende

''Baada ya miezi saba ya uchunguzi, ndio wamekuja kutuambia kwa urahisi wote kwamba Okende alijiua. Kwamba waligundua maandishi yake kwenye afisi yake akisema alikerwa na maisha yake," alisema Dewaef.

"Ni jambo lisilo ingia kilini. Ni lini waligundua maandishi hayo? Ni taafira gani waliyo nayo ambayo inahitimisha kujiua kwamba alijiuwa ? waliipata toka muda gani? Kwa nini basi walisubiri muda mrefu ili kuwasiliana na familia? Ni nini matokeo ya uchunguzi wa maiti wa Agosti 3 ? haya maswali yote lazima mtu ayajibu,'' alisisitiza.

Lucha: 'Hii ni kashfa na upuuzi'

Kwa upande wake, vuguvugu la kuunga mkono demokrasia nchini Kongo, Lucha, pia lilisema kwamba hitimisho la uchunguzi wa mahakama ni kashfa na upuuzi kabisa. Mashirika ya kutetea haki za binadamu nchini pia yalikuwa kwenye mustari wa mbele kulalamikia ripoti hiyo ambayo wamesema ni aibu kwa taifa la haki.

Familia ya Cherubin Okende ikiwa imekatishwa tamaa na ucheleweshaji wa vyombo vya sheria vya Kongo, ilitangaza Februari 1 uamuzi wake wa kumzika ili kumaliza maombolezo, bila kungoja hitimisho la ripoti ya uchunguzi wa maiti kutoka kwa mwendesha mashtaka. Hadi kufikia sasa mwili wa Okende bado kuzikwa.

Cherubin Okende, aliyekuwa wa waziri wa uchukuzi alijiuzulu chini ya Rais Felix Tshisekedi kama mwanachama wa chama cha mpinzani mkuu Moise Katumbi. Wakati huo, Katumbi alikuwa ametangaza nia yake ya kugombea urais na kukiondoa chama chake katika muungano na chama cha rais Tshisekedi.

Nyaraka za siri za idara ya upelelezi ambazo zilidukuliwa na vyombo vya habari zilionyesha kuwa Okende alitekwa nyara na maafisa wa idara za usalama wa jeshi, kabla ya kukutwa amefariki siku moja baadae. Hadi kufikia sasa mwili wa Okende bado kuzikwa.