Fabrice Muamba aonyesha dalili za kuimarika | Michezo | DW | 20.03.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Fabrice Muamba aonyesha dalili za kuimarika

Klabu ya Bolton Wanderers imesema kiungo wake anayeugua Fabrice Muamba sasa anaweza kupumua mwenyewe lakini angali katika hali mbaya. Muamba yuko katika hospitali ya London Chest nchini Uingereza.

Bolton Wanderers manager Owen Coyle (L) walks alongsde the stretcher as medical staff attend to Fabrice Muamba after he collapsed on the pitch during their FA Cup quarter-final soccer match against Tottenham Hotspur at White Hart Lane in London March 17, 2012. Tottenham Hotspur's FA Cup quarter-final against Bolton Wanderers was abandoned on Saturday after Bolton midfielder Fabrice Muamba collapsed near the centre circle. REUTERS/Suzanne Plunkett (BRITAIN - Tags: SPORT SOCCER)

Fußball England Zusammenbruch Fabrice Muamba

Katika taarifa ya pili kutoka kwa klabu hiyo ya ligi kuu ya soka Uingereza, ni kuwa Muamba anaendelea kuonyesha dalili za kuimarika, siku mbili tu baada ya kupatwa na mshtuko wa moyo wakati wa mchuano wao wa kombe la FA. Taarofa hiyo ilisema sasa anaweza kupumua kwa kujitegemea bila usaidizi wa mitambo. Pia anaweza kuwatambua watu wa familia yake na kuyajibu maswali ipasavyo.

Fabrice Muamba alipatwa na mshtuko wa moyo wakati wa mechi ya Tottenham na Bolton

Fabrice Muamba alipatwa na mshtuko wa moyo wakati wa mechi ya Tottenham na Bolton

Wakati huo huo mtaalamu mmoja wa upasuaji wa moyo amesema atawafanyia vipimo wachezaji wa klabu ya Tottenham Hotspurs ili kuona kama kuna uwezekano wa matatizo yoyote ya moyo, kutokana na ombi la wachezaji waliomuona kiungo wa Bolton Fabrice Muamba akipatwa na mushtuko wa moyo na kuzirai uwanjani. Daktari wa moyo Sanjay Sharma amesema matukio ya mushtuko wa moyo miongoni mwa vijana ni nadra sana, na humwathiri mmoja kati ya watu 50,000. Maradhi mengi ya moyo ni ya urithi kutoka kwa kizazi kimoja hadi kingine.

Huku hayo yakijiri, mchuano wa ligi ya Uingereza kati ya Bolton Wanderers nyumbani kwa Aston Villa uliotarajiwa kuchezwa kesho umeahirishwa kutokana na hali ya Muamba. Maafisa wa ligi wamesema mchuano huo umeahirishwa kutokana na ombi la klabu ya Bolton. Wachezaji wa Bolton hawako tayari kucheza mchuano huo na hivyo utapangwa tena baadaye. Mchuano utakaofuata utakuwa dhidi ya Blackburn Rovers siku ya Jumamosi.

Dortmund na Bayern wapepea

Katika ligi ya soka Ujerumani – Bundesliga, mabingwa Borussia Dortmund waliendelea kuongoza kwa tofauti ya pointi tano baada ya ushindi wao wa goli moja bila jawabu mwishoni mwa wiki dhidi ya Werder Bremen.

Dortmund wanaendelea kushika usukani wa Bundesliga

Dortmund wanaendelea kushika usukani wa Bundesliga

Bayern Munich waliwazaba Hertha Berlin magoli sita kwa sifuri na kusalia katika nafasi ya pili na pointi 54. Nambari tatu Borussia Moenchengladbach iliyo na pointi 52 inaendelea kutafuta tiketi ya kushiriki ligi ya mabingwa msimu ujao, baada ya kuwafunga Bayer Leverkusen magoli mawili kwa moja. Schalke pia wanaendelea kudhihirisha umahiri wao baada ya kuwaduwaza Kaiserslautern mabao manne kwa moja jana Jumapili.

Wakati huo huo Bayern Munich na Borussia Dortmund wataendeleza vita vya ubabe wao katika soka ya nyumbani kuwania kombe la shirikisho la Ujerumani, DFB Pokal wakilenga kukutana katika fainali. Mabingwa wa ligi na ambao ni viongozi Dortmund watasafiri kuchuana na klabu ya daraja la pili Greuther Fuerth katika nusu fainali ya kwanza kesho Jumanne. Kisha Jumatano mabingwa watetezi wa taji hilo Bayern Munich watakuwa nyumbani kwa mahasimu wao wa Bundesliga Borussia Moenchengladbach katika nusu fainali ya pili. Fainali itakuwa Mei 7 katika uwanja wa Olimpiki jijini Berlin.

Saudi Arabia kuwatuma wanawake katika Olimpiki

Nembo ya michezo ya Olimpiki jijini London 2012

Nembo ya michezo ya Olimpiki jijini London 2012

Saudi Arabia inatarajiwa kuwatuma wanariadha wanawake katika mashindano ya Olimpiki kwa mara ya kwanza mwaka huu. Saudi Arabia, Brunei na Qatar hawajawahi kuwajumuisha wanariadha wa kike katika timu zao na Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki IOC, ina hamu ya kuona hali hiyo ikibadilika jijini London mwezi Julai.

IOC imesema leo kuwa maafisa wa Kamati ya Olimpiki ya Saudi Arabia wamewasilisha orodha ya wanariadha wa kike wanaoweza kushiriki mashindano hayo ya Olimpiki jijini London.

Shirika la haki za binaadamu la Humans Rights Watch liliwashutumu waandalizi wa michezo ya Olimpiki kwa kile lilichokitaja kuwa ni ubaguzi wa kijinsia kutoka mataifa ya Ghuba ya Kiarabu ya Saudi Arabia na Qatar, pamoja na nchi ndogo ya Kusini Mashariki mwa Asia Brunei. Qatar inayowania fursa ya kuandaa mashindano ya Olimpiki mwaka 2020, ilisema itawatuma wanariadha wanawake katika mashindano ya Olimpiki London kwa mara ya kwanza.

Mwandishi: Bruce Amani/Reuters/AFP/DPA

Mhariri: Josephat Charo