1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Euro Bilioni 700 kuukabili mgogoro wa madeni

31 Machi 2012

Nchi za Umoja wa sarafu ya Euro zimepiga hatua zaidi mbele katika juhudi za kukabiliana na mgogoro wa madeni baada ya kufikia makubaliano ya kuongeza fedha katika mfuko wa uokozi.

https://p.dw.com/p/14VdX
Participants of the Ecofin Finance Minister meeting pose for media during a group photo in Copenhagen, March 30, 2012. REUTERS/Fabian Bimmer (DENMARK - Tags: POLITICS BUSINESS)
Dänemark Ecofin GruppenbildPicha: Reuters

Mawaziri wa fedha wa nchi zinazotumia sarafu ya Euro wamekubaliana kuongeza uwezo wa kifedha hadi Euro Bilioni 700 ili kuepusha migogoro mingine ya madeni kutokea katika nchi zao. Masoko na washirika wa nchi za G 20 wamezipokea habari hizo kwa faraja.

Mawaziri hao wa nchi 17 za Umoja wa sarafu ya Euro wameamua kuiunganisha mifuko miwili ya uokozi na hivyo kupata Euro Bilioni 500 zitakazowekwa tayari kuikabili dharura yoyote itakayotokea baina ya sasa na kati kati ya mwaka ujao. Fedha hizo ni nyongeza ya Euro Bilioni 200 ambazo zimekwishawekwa tayari kwa ajili ya kuziokoa Ugiriki, Ireland na Ureno.

Mkurugenzi wa Shirika la Fedha la Kimataifa, IMF Christine Lagarde ameafikiana na uamuzi huo na amesema kuwa utalisaidia shirika lake, linalotoa mikopo duniani, kuweza kuongeza fedha ili kuzuia kuenea kwa athari zinazotokana na mgogoro wa madeni barani Ulaya, ikiwa litahitajika kufanya hivyo

Mkurugenzi wa IMF Christine Lagarde na Waziri wa fedha wa Ujerumani Wolfgang Schäuble
Mkurugenzi wa IMF Christine Lagarde na Waziri wa fedha wa Ujerumani Wolfgang SchäublePicha: AP

Kutokana na shinikizo la kimataifa kuwataka waukabili mgogoro wa madeni ambao umeshachukua muda wa miaka miwili na kutokana na matatizo ya bajeti ya Uhispania ,mawaziri hao wamefikia makubaliano yenye lengo la kuyapa imani masoko ya fedha.

Marekani imesema makubaliano ya mawaziri wa nchi za Umoja wa Sarafu ya Euro yameimarisha imani katika eneo la Euro.Msemaji wa wizara ya fedha ya Marekani ameeleza kuwa, katika miezi kadhaa iliyopita viongozi wa Ulaya wamepiga hatua madhubuti katika kuukabili mgogoro wa madeni.

Mwandishi:Mtullya Abdu/AFP

Mhariri:Bruce Amani