Erdogan: Tunakemea matukio ya kibaguzi uwanjani | Michezo | DW | 09.12.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Erdogan: Tunakemea matukio ya kibaguzi uwanjani

Rais wa Uturuki Tayyip Erdogan amesema kuwa tukio la kibaguzi katika mechi ya klabu bingwa barani Ulaya kati ya Paris St Germain na Istanbul Basaksehir ni muendelezo wa matukio ya kibaguzi yanayoendelea nchini Ufaransa.


Erdogan ameuambia mkutano wa waandishi habari mjini Ankara: "Tukio hilo la kibaguzi haliwezi kusamehewa kabisa. Msimamo wetu wa kukabiliana na ubaguzi bado ni ule ule na utaendelea. Ufaransa ni moja kati ya nchi zenye kuendekeza matukio ya kibaguzi."

Jana Jumanne 08.12.2020, wachezaji wa Istanbul Basaksehir na Paris St Germain waliondoka uwanjani baada ya klabu hiyo ya Uturuki kumshtumu msimamizi mmoja wa mechi hiyo Sebastian Coltescu, kwa kutumia neno la kibaguzi kwa kocha msaidizi wa Basaksehir Pierre Webo, ambaye ni mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya Cameroon.

Mshambuliaji wa PSG Kylian Mbappe aliandika kwenye ukurusa wake wa Twitter: "Tunapinga Ubaguzi. Webo, tuko na wewe katika hili." 

Gazeti la michezo la Uturuki la Fotomac limesema tukio hilo la kibaguzi limetia doa nyeusi kwa mchezo wa soka.

Shirikisho la soka barani Ulaya UEFA limeahidi kuchunguza tukio hilo.