1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Historia

Eduardo Mondlane: Muasisi wa umoja wa kitaifa wa Msumbiji

Yusra Buwayhid
11 Februari 2020

Eduardo Mondlane alikuwa na ndoto ya kupatikana Msumbiji iliyo huru na yenye umoja, bila ya vizuizi vya wakoloni wa Ureno. Licha ya kuuliwa, aliwacha urithi utakaokumbukwa daima.

https://p.dw.com/p/3XJoD

Eduardo Mondlane: Kiongozi aliyeiunganisha Msumbiji

Eduardo Mondlane alizaliwa wapi na lini? Eduardo Chivambo Mondlane alizaliwa Juni 20, 1920, Manjacaze, mkoa wa Gaza, kusini mwa Mozambique. Alifnya kazi kama mchungaji hadi alipotimiza umri miaka 10. 

Wapi Eduardo Mondlane aliipata elimu yake? Mondlane kwanza alisoma katika shule ya msingi ya wamishionari wa Uswisi iliyokuweko karibu na Manjacaze na baadae alisomea Anthropolojia na sosholojia nchini Afrika Kusini na baade (kwa muda mfupi) nchini Ureno. Alikutana na viongozi wa Kiafrika wa vuguvugu la kupinga ukoloni akiwa Afrika Kusini, kama vile Amílcar Cabral wa Guinea-Bissau na Angola's Agostinho Neto wa Cape Verde.

African Roots  | Eduardo Mondlane
DW Asili ya Afrika | Eduardo Mondlane

Baadae alikwenda Marekani kuchukua shahada ya juu kabisa ya masomo hayo (shahada ya udaktari). Akiwa Marekani, Mondlane alisomesha katika Chuo Kikuu cha Syracuse na baadae alijiunga na Baraza la Udhamini la Umoja wa Mataifa kama mtafiti wa masuala yanayohusiana na Uhuru wa nchi za Kiafrika. Miongoni mwa mambo mengine alihusika katika maandalizi ya kura ya maoni ya upande wa Cameroon unaozungumza Kiingereza mwaka 1961, ambayo baadae itakuja kuamua utenganisho wa mipaka kati ya Nigeria na Cameroon.

Eduardo Mondlane anajulikana zaidi kwa lipi? Alikuwa ni rais wa kwanza na mwanzilishi mwenza wa vuguvugu la ukombozi wa Msumbiji FREMOLIMO (Mozambican Liberation Front) jijini Dar es Salaam, Tanzania, mnamo mwaka 1962, vuguvugu ambalo baada ya kifo cha Mondlane, liliendeleza hatarakati zake hadi ukapatikana uhuru. Mondlane alikuwa ni mwanamapinduzi anaeunga mkono mshikamano wa watu wa asili ya Kiafrika, mtaalamu wa masuala ya kimataifa pamoja na somo la Anthropolojia ambayo ni elimu inayochunguza pande zote za binadamu kuanzia jamii za watu wa kale.

Eduardo Mondlane anaheshimiwa kwa lipi? Hadi hii leo, Mondlane anaheshimiwa na wengi kwa kuwa na maono ya mbali ya kuliunganisha taifa la Msumbiji, yaliyosaidiwa na sifa zake nzuri za kielimu.

Eduardo Mondlane: Kiongozi aliyeiunganisha Msumbiji

Vipi kilitokea kifo cha Eduardo Mondlane? Mnamo Febuari 3, 1969, Mondlane aliuliwa mjini Dar es Salaam alipofungua kifurushi kilichokuwa kimetegwa bomu ndani yake. Kuna baadhi wanaowanyooshea kidole cha lawana wapinzani wake ndani ya FRELIMO na PIDE, Jeshi la Ulinzi la Kimataifa la Taifa la Ureno. Lakini hadi hii leo, mauaji yake bado ni kitendawili.

Je, Eduardo Mondlane aliandika vitabu vyovyote? Eduardo Mondlane aliandika vitabu vingi miongoni mwao 'Lutar por Moçambique' (Harakati za Msumbiji), kilichotolewa muda mfupi baada ya kifo chake. Kinachukuliwa kuwa kitabu muhimu sana kwa vuguvugu hilo la kitaifa.

Serikali ya Msumbiji inamkumbukaje Eduardo Mondlane? Chuo Kikuu cha Lourenço Marques, katika mji mkuu wa Msumbiji wa Maputo, ambacho awali kilipewa jina hilo na utawala wa Ureno, kilibadilishwa jina na kuitwa Chuo Kikuu cha Eduardo Mondlane baada ya uhuru mwaka 1975.

Ushauri wa kisayansi kuhusu makala hii umetolewa na wanahistoria Profesa Doulaye Konaté, Lily Mafela, Ph.D., na Profesa Christopher Ogbogbo. Mfululizo wa makala za Asili ya Afrika umefadhiliwa na Taasisi ya Gerda Henkel.