1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ECOWAS yaziondolea vikwazo Mali na Burkina Faso

4 Julai 2022

Viongozi wa Afrika Magharibi waliokuwa wakihudhuria mkutano wa kilele wa kanda hiyo wameamua kuziondolea vikwazo vyote vya kifedha na kiuchumi Mali na Burkina Faso.

https://p.dw.com/p/4DbJP
Afrika ECOWAS Gipfel
Picha: FRANCIS KOKOROKO/REUTERS

Haya yamesemwa na Jean Claude Kassi Brou, mwanasiasa wa Ivory Coast ambaye amekuwa akihudumu kama rais wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi ECOWAS.

Brou lakini amesema nchi hizo mbili bado zimefungiwa uanachama wake wa ECOWAS. Rais huyo amesema Guinea bado haijaondolewa vikwazo vyovyote vile kwa kuwa haikuwasilisha mkakati uliokubalika utakaoipelekea nchi hiyo kufanya uchaguzi utakaorudisha utawala wa kiraia.

Brou ameeleza kuwa nchi zote tatu zitarudi kuwa wanachama wa Jumuiya hiyo ya Afrika Magharibi mara tu zitakapofanya uchaguzi.

Kuathirika vibaya kwa uchumi kutokana na vikwazo vya fedha

Jeshi la Mali limeahidi kufanya uchaguzi mnamo Machi 2024 pendekezo lililokubaliwa ingawa mjumbe mmoja wa ECOWAS amesema hakuna mwanajeshi yeyote atakayekubaliwa kugombea urais katika uchaguzi wowote ujao nchini Mali.

Afrika ECOWAS Gipfel
Wakuu wa ECOWAS wakihudhuria mkutano wa kilele JumapiliPicha: FRANCIS KOKOROKO/REUTERS

Mali iliwekewa vikwazo vya kibiashara na kifedha mnamo mwezi Januari, jambo lililopelekea nchi hiyo maskini ambayo haina bahari na ambayo uchumi wake ni duni tayari kutokana na mapigano ya kijihadi yaliyodumu kwa miongo kadhaa.

Nalo jeshi la Burkina Faso limeomba kipindi cha mpito cha miaka miwili kabla kufanya uchaguzi. Jeshi hilo vile vile limesema litafanya kura ya maoni ya katiba mwezi Desemba mwaka 2024 na uchaguzi wa bunge na rais Februari 2025.

Akiizuru Ouagadougou kwa mara ya kwanza katika kipindi cha mwezi mmoja, mpatanishi wa ECOWAS Mahamadou Issoufou alimsifu mkuu wa jeshi Luteni Kanali Paul-henri Sandaogo Damiba na serikali yake kwa uwazi wao katika majadiliano.

Issoufou ambaye ni rais wa zamani wa Niger amesema hali ya kiongozi aliyeondolewa madarakani Roch Marc Christian Kabore pia imejadiliwa. Vyama vya kisiasa vinavyomuunga mkono Kabore vimeupinga mpango huo wa jeshi la Burkina Faso vikisema havikushauriwa mapema.

Wimbi la mapinduzi Afrika Magharibi

Huko Guinea hali inaonekana kuwa ngumu zaidi kwa kuwa jeshi la nchi hiyo limemkataa mpatanishi wa ECOWAS na likatangaza kipindi cha mpito cha miezi 36. Rais wa Senegal ambaye pia ndiye rais wa Umoja wa Afrika Macky Sall ameelezea kipindi hicho cha mpito kama kisochoweza kufikirika.

Mali Präsident Oberst Assimi Goita
Rais wa Mali Kanali Assimi GoitaPicha: Habib Kouyate/Xinhua/IMAGO

Utawala wa kijeshi wa Guinea umefanya juhudi za kukutana na vyama vikuu vya upinzani nchini humo ila vyama hivyo vimekataa kwa sharti la kuwa, kushiriki kwao ni mpaka pale patakapoteuliwa mpatanishi wa ECOWAS.

Wimbi la mapinduzi Afrika Magharibi lilianza Agosti 2020 pale Kanali Assimi Goita na majeshi wengine walipomuondoa rais wa Mali aliyechaguliwa kidemokrasia . Miezi tisa baadae, Kanali Goita akafanya mapinuzi mengine nchini humo ambapo aliuondoa madarakani uongozi wa mpito wa kiraia na kuchukua urais mwenyewe.

Huko Guinea wanajeshi walimuondoa madarakani rais mnamo Septemba 2021 na mnamo januari Roch Christian Kabore wa Burkina Faso akapinduliwa.

Chanzo: AFP/AP