1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroSudan

DRC yasema raia wake 10 wameuawa mjini Khartoum

Daniel Gakuba
6 Juni 2023

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imesema raia wake 10 wameuawa nchini Sudan, wakati jeshi la Sudan lilipokishambulia chuo kikuu mjini mjini Khartoum wakati hali ikiendelea kuwa tete.

https://p.dw.com/p/4SFtD
Sudan | Khartoum
Picha: Mohamed Nureldin Abdallah/REUTERS

Waziri wa mambo ya nje wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo, Christophe Lutundula amewaambia waandishi wa habari kuwa raia 10 wa Kongo waliuawa katika mashambulizi ya mabomu kwenye chuo kikuu mjini Khartoum Jumapili iliyopita.

Amesema mashambulizi hayo yaliyofanywa na jeshi la serikali ya Sudan katika maeneo ya raia, wakiwemo kutoka mataifa ya nje, yalijeruhi pia raia kadhaa wa Kongo.

Waziri huyo wa mambo ya nje wa Kongo, amesema amemuita afisa wa ubalozi wa Sudan mjini Kinshasa, kulalamikia mauaji ya wanafunzi wa Kongo, na kumuuliza kinachofanyika ili miili ya marehemu isafirishwe kurudi nyumbani Kongo.

Mapigano yaliyodumu kwa wiki saba sasa, kati ya jeshi la Sudan na wanamgambo wa RSF yamekwishauwa watu zaidi ya 1800, na kuwalazimisha zaidi ya milioni moja kuyahama makaazi yao.

Wakati huo huo simulizi za wakaazi wa mji wa Khartoum zinaeleza kuwa milio mizito ya mizinga ilisikika mjini humo, huku vitendo vya ukiukaji wa sheria vikizidi kusambaa mjini humo.

Machafuko yalienea hadi Omdurman, mji pacha na Khartoum kwenye ukingo mkabala wa mto Nile, ambako mapigano ya ardhini kati ya makundi yanayohasimiana ni vya nadra.

Sudan | Mapigano mjini Khartoum
Raia wakipita kando ya jengo la hospitali liliporomoshwa na milipuko ya silaha mjini KhartoumPicha: AFP/etty Images

Mkaazi mmoja wa Omdurman, Mohamed Saleh, amesema vitendo vya uhalifu na uporaji vimekuwa vikiendelea mchana kweupe kila siku, bila juhudi zozote za vyombo vya usalama kuingilia kati.

Waleed Adam ambaye anakaa upande mwingine wa Mto Nile, amesema wapiganaji wa RSF wamesambaa katika vitongoji vyao na kuchukua udhibiti kamili, huku wakipora kila kitu.

Ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa huwa anawaona kila siku wakichukua kila kitu wanachokiona, kuanzia magari, fedha na dhahabu, na akielezea hofu yake kuwa ni suala la muda tu hatimaye zamu yake ya kuporwa itafika.Mapigano yaendelea kushuhudiwa nchini Sudan

Ghasia hizi nchini Sudan zimezidisha makali ya mzozo wa kibinadamu katika mataifa jirani kama Chad na Jamhuri ya Afrika ya Kati, ambayo ilikuwa mbaya hata kabla ya mzozo huo kuibuka. Alipokuwa akizungumza mjini Geneva jana Jumatatu, msaidizi wa mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, Mohammed Ag Ayoya, alisema wakimbizi kutoka Sudan wamezorotesha zaidi hali katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, ambako kati ya kila watu watano, mmoja amelazimika kuyakimbia makaazi yake kutokana na vurugu zinazofanywa na makundi yenye silaha.