1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

DRC yafanya uchaguzi wa maseneta.

Mitima Delachance (Mhariri: Grace Patricia Kabogo)15 Machi 2019

Maseneta 100 wamechaguliwa katika majimbo 24 ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo. Kila jimbo limewachagua maseneta 4 na jimbo la Kinshasa maseneta 8.

https://p.dw.com/p/3F8uR
DR Kongo Parlament außen in Kinshasa
Picha: Getty Images/AFP/J.D. Kannah

Uchaguzi wa Baraza la Seneti umefanyika leo Ijumaa katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo. Uchaguzi huo unawahusisha jumla ya maseneta mia moja na nane kutoka kwenye majimbo yote ya nchi hiyo. Uchaguzi huo unafanyika kukiwa na lawama za ushawishi wa kikabila.

Kwa fursa hii ni maseneta mia moja waliochaguliwa katika majimbo ishirini na nne ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo. Kila jimbo limewachagua maseneta wanne na jimbo la Kinshasa maseneta wanane. Hata hivyo, hadi sasa, bado uchaguzi wa wabunge haujafanyika katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Maindombe, ambako maseneta wengine wanane watatoka huko.

Katika Kivu Kusini, Pierre Lumbi, akiwa mgombea wa chama cha Lamuka cha Martin Fayulu amechaguliwa, na wagombea watatu wengine ni kutoka muungano wa FCC unaovihusisha vyama vinavyomuunga mkono rais aliyeondoka madarakani Joseph Kabila.

Uchaguzi wa maseneta unafanyika wakati huu kukiwa na baadhi ya wakaazi wa Kivu Kusini kutoka kabila za "Balega”, wanaonyoosha kidole cha lawama kuhusu uchochezi wa ukabila katika harakati zote za uchaguzi tangu Desemba 30. Na kama inavyoonekana kwa mara nyingine tena, hakuna mtu wa kabila hilo aliyechaguliwa.

Uchaguzi wa maseneta umefanyika kukiwa na lawama za ushawishi wa kikabila.
Uchaguzi wa maseneta umefanyika kukiwa na lawama za ushawishi wa kikabila.Picha: Getty Images/AFP/J. Wessels

Miongoni mwa viongozi wa kabila hili wanaokerwa na suala hilo ni pamoja na Jean-Marie Bulambo Kilosho, mbunge wa kitaifa ambaye kwa sasa yuko ziarani mjini Bukavu. Kilosho anahisi kwamba baadhi ya wabunge wameshawishiwa na viongozi walioko Kinshasa.

Hali hii imesababisha baadhi ya vijana wa kabila hili la Balega kuonesha nia yao ya kulitaka jimbo hili la Kivu Kusini ambapo tayari zaidi ya saini laki moja na themani na sita zimekusanywa, kwa lengo la kuibadili hali iliyopo. Mbunge Bulambo Kilosho anafafanua zaidi.

Ombi hili linatupiliwa mbali na asasi nyingi za kiraia hapa Kivu Kusini. Zozo Sakali ni mwanasheria na pia kiongozi wa asasi ya kiraia mjini Bukavu.

Baada ya uchaguzi huu wa maseneta, uchaguzi wa magavana wa majimbo unapangwa kufanyika Machi 26.