Dick Cheney azuru Georgia | Matukio ya Kisiasa | DW | 04.09.2008
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Dick Cheney azuru Georgia

Marekani iko nyuma ya Georgia katika changamoto yake na Urusi.

Dick Cheney na Saakashvili

Dick Cheney na Saakashvili

Makamo-rais wa Marekani Dick Cheney,akiwa ziarani mjini Tibilisi,Georgia,aliahidi kuwa Marekani iko nyuma ya Georgia katika changamoto yake na Urusi.Aliueleza uvamizi wa Urusi katika nchi hiyo ya zamani ya kisoviet si "halali"-kitendo ambacho alisema kinatia dosari kubwa juu ya uaminifu wa Urusi.

Dick Cheney,anaechukua msimamo mkali na mmoja kati ya wakosoaji wakubwa wa siasa za Urusi,ndie mjumbe wa hadhi ya juu kabisa wa marekani kutembelea Georgia tangu Georgia kujaribu kulikomboa kwa nguvu jimbo lake Ossetia kusini mapema August na halafu kuvamiwa na majeshi ya urusi.

Maneno yake makali kama desturi yake, yamkini yakaiudhi Kremlin ilioituhumu Marekani kupalilia moto kwa kumkumbatia rais Mikhail Saakashvilli wa Georgia,mwanasheria alieelimishwa Marekani na mwenye usuhuba mwema na utawala wa rais George Bush.

Cheney alisema na ninamnukulu,

"Baada ya nchi yenu kujipatia uhuru katika mapinduzi ya waridi,Marekani ilikuja kusaidia demokrasia hii changa na ya kishujaa ."

Hapo Cheney akigusia mapinduzi ya amani yaliotokea Georgia hapo 2003 yaliomleta madarakani Saakashvili.

Cheney akaongeza,

"Tunafanya hivyo tena hivi sasa unapojitahidi kuzima uvamizi wa mamlaka yako huru pamoja na kuzuwia jaribio lisilo halali ,la upande mmoja kubadili mipaka ya nchi yako kwa nguvu-jambo ambalo limelaaniwa na ulimwengu huru."

Cheney akiihakikishia Georgia msaada wa Marekani alisema,

"Kama nilivyomhakikishia rais Sakashvili leo,Marekani itaisaidia Georgia kujenga upya ili ichukue tena nafasi yake kama nchi inayokuza haraka uchumi wake."

Ni jana tu pale waziri wa nje wa Marekani dr.Condoleeza Rice aliponadi:

"Ninafuraha kutangaza msaada mkubwa wa Marekani wa si chini ya dala bilioni 1 ili ikidhi mahitaji yake makubwa na kurahisisha kuujenga upya uchumi wake."

Dick cheney, akiwa katika ziara ya washirika i katika eneo la Kaukasus ilioanza jana (jumatano) nchini Azerbaijan,alisema hatua za Urusi zimezusha shaka shaka kubwa kuhusu nia na uaminifu wake kama mshirika tena tangu katika eneo hilo hata kimataifa.

Tangu Azerbaijan hata Georgia zimeunganishwa katika mlolongo wa nchi zinazozalisha nishati znazoegemea magharibi na kuikwepa Urusi.Mlolongo huo unaohifiwa kuingia sasa hatarini kutokana na uvamizi wa urusi nchini Georgia.

Moscow imejibu kwamba imeingia Georgia kuzuwia ilichokiita "mauaji ya kuhilikisha umma pale Tibilisi ilipoanzisha hujuma zake kuiteka Ossetia kusini,inayoelemea Urusi,hapo August 7. Moscow baadae ikaitambua osseti kuwa nchi huru pamoja na Abkhazia-jimbo la pili lililojitenga na Georgia.Hii ililaaniwa na Washington na washirika wake wa Ulaya.Ni Nicaragua tu ilioifuata Urusi kuyatambua maeneo hayo 2 kama nchi huru.

Kabla Dick Cheney hakuruka kwa safari ya Ukraine-ambayo kama Georgia -nchi ya zamani ya kisoviet-inayolilia uwanachama wa NATO,Dick Cheney, alipashwa habari juu ya juhudi za uokozi na misaada .Akaangalia ndege ya Marekani chapa C 130 ikipakia mablangeti,chakula na shehena nyengine kupeleka sehemu ya kijeshi ya uwanja wa ndege wa Tibilisi.

Uwanja huo ulihujumiwa kwa mabomu na Urusi mwezi uliopita.

Maafisa wa Marekani wanasema kuwa misaada ya kibinadamu ya Marekani inayofikia dala milioni 37 imeshawasili Georgia tangu vita kuripuka mwezi uliopita.

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com