Daktari: Schumacher aendelea kuimarika | Michezo | DW | 24.10.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Daktari: Schumacher aendelea kuimarika

Michael Schumacher huenda akapona katika kipindi cha miaka mitatu. Hayo ni kwa mujibu wa daktari Mfaransa anayemtibu dereva huyo wa zamani bingwa wa mashindano ya magari ya Formula One.

Dereva huyo Mjerumani anaendelea vyema kupata nafuu ila taratibu mno, ikiwa ni miezi kumi baada ya kuhusika katika ajali mbaya kabisa ya mchezo wa kuteleza kwenye theluji.

Daktari Jean-Francois Payen ameiambia redio ya RTL amesema Schumi anaendelea kupata nafuu isipokuwa hali yake inahitaji subira. Payen alimtibu Schumacher baada ya kuhusika katika ajali, katika hospitali ya mji wa Grenoble nchini Ufaransa, na sasa anafuatilia hali yake nyumbani kwa dereva huyo mjini Gland, Uswisi pamoja na hospitali nyingine ya Lausanne.

Michael Schumacher ndiye dereva aliyepata mafanikio makubwa zaidi katika historia ya Formula One. Kando na Mataji yake ya Ubingwa wa Dunia, Shumacher pia alishiriki katika mashindano makuu 308 ya Grand Prix. Kwanza alistaafu mwaka wa 2006, lakini akarejea tena katika mchezo huo miaka mitatu baadaye, ijapokuwa alipata mafanikio madogo. Baada ya msimu wa 2012, alistaafu kabisa kutoka ulimwengu wa Formula One.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/reuters
Mhariri: Yusuf Saumu