1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Croatia yatinga fainali ya Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza

Bruce Amani
12 Julai 2018

Croatia imetinga katika fainali ya Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza katika historia yao baada ya bao la ushindi katika muda wa ziada la Mario Mandzukic kuizamisha England kwa mabao 2-1

https://p.dw.com/p/31JOE
WM 2018 - Kroatien - England
Picha: imago/Agencia EFE/L. Deirax

Timu hiyo ya Luka Modric ilijikuta ikiwa nyuma baada ya dakika tisa tu kutokana na bao safi sana la mkwaju wa freekick uliopigwa na Kieran Trippier, lakini wakasawazisha kupitia Ivan Perisic kabla ya Mandzukic kuwapa ushindi wa mabao mawili kwa moja mbele ya mashabiki 78,000 katika uwanja wa Luzhniki, mjini Moscow.

Kwa kuizaba timu changa ya kocha Gareth Southgate, Croatia – nchi ya idadi ya watu milioni nne tu – wameyapita mafanikio ya mashujaa wa mwaka wa 1998, ambao walitinga katika nusu fainali nchini Ufaransa na kuondolewa na wenyeji Ufaransa.

Wachezaji wa Croatia walisherehekea mbele ya mashabiki wao mjini Moscow wakati mjini Zagreb, maelfu ya mashabiki walimiminika mitaani na mabarabarani wakiimba na kupeperusha bendera za rangi nyeupe, nyekundu na bluu.

Baada ya kuwa kifua mbele kwa Zaidi ya saa moja, kichapo hicho kitakuwa kigumu kwa England kutafakari wakati matumaini yao ya kufika fainali ya kwanza ya Kombe la Dunia tangu mwaka wa 1966 yalikatizwa, lakini timu yao changa imepata mashabiki wengi nchini Urusi.

Fußball WM 2018 Kroatien vs England
Shangwe mjini Zagreb baada ya ushindi wa CroatiaPicha: Reuters/A. Bronic

Croatia lazima wajiandae haraka kwa fainali kali ya Jumapili – kitu ambacho sio rahisi baada ya kufikishwa katika muda wa ziada kwa mechi ya tatu mfululizo. Lakini Kocha Zlatko Dalic anaamini kuwa uchovu hautaiathiri timu yake wakati itakapopambana na Ufaransa.

Ivan Perisic ambaye ndiye alikuwa mchezaji bora wa mechi ya jana, alisema ulikuwa mchezo mgumu, na kila mmoja alifahamu umuhimu wa nusu fainali kwa nchi ndogo kama Croatia.

Wachezaji wa England walianguka uwanjani baada ya kipyenga cha mwisho kupulizwa, wasiweze kuamini ndoto yao ya Kombe la Dunia imeisha baada ya kufika nusu fainali kwa mara ya kwanza tangu mwaka wa 1990.

Harry Kane, ambnaye huenda akashinda tuzo ya mfungaji bora wa mashindano hayo akiwa na mabao sita nchini Urusi, alisema wamehuzunishwa na kichapo hicho lakini watajivunia mafanikio yao.

Fußball WM 2018 Kroatien vs England
Ndoto ya England ilikatizwa na uzoefu wa CroatiaPicha: Reuters/J. Super

Kocha Southgate alielezea kusikitishwa kwake lakini akawapongeza wachezaji wake kwa namna walivyojituma katika mashindano hayo.  

Mjini London, msisimko wa awali uligeuka kuwa huzuni wakati mashabiki 30,000 waliofurika katika uwanja wa Hyde Park walishuhudia timu yao ikishindwa.

Karibu watu milioni 30 wanaaminika kuutazama mtanange huo kwenye televisheni nchini Uingereza. Mwanamfalme William, rais wa Shirikisho la Kandanda alisema licha ya kichapo hicho England inajivunia timu hiyo ya kocha Southgate

Ufaransa wana faida ya kupumzika kwa siku moja Zaidi ya wapinzani wao baada ya kujikatia tikiti ya fainali kwa mara ya tatu katika historia yao siku ya Jumanne. Waliwazidi nguvu Ubelgiji kwa kuwafunga bao moja kwa sifuri. Ubelgiji na England sasa zitakutana Jumamosi katika mchuano wa kuamua mshindi wa nafasi ya tatu

Barabara kabisa mambo ni kama ulivyoyasikiliza kutoka kwa Bruce Amani.

Mwandishi: Bruce Amani
Mhariri: Iddi Ssessanga