1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vipimo vya lazima katika uwanja wa ndege

23 Julai 2020

Wasafiri wanaoingia Ujerumani kutoka nchi zilizoathirika zaidi na janga la virusi vya Corona watalazimika kufanyiwa vipimo vya kubaini iwapo wameambukizwa virusi hivyo katika viwanja wa ndege.

https://p.dw.com/p/3flHF
Fluggesellschaft Condor
Picha: Getty Images/AFP/I. Fassbender

Mawaziri wa afya katika majimbo yote ya Ujerumani wameafikiana kwa kauli moja kuwa itamlazimu kila mtu anayeingia Ujerumani kufanyiwa vipimo vya kubaini iwapo wameambukizwa virusi vya Corona au la katika viwanja vya ndege.

Mawaziri hao wa afya wa majimbo pamoja na waziri wa afya katika serikali kuu Jens Spahn walifikia uamuzi huo baada ya kufanya mkutano kwa njia ya mtandao jana Jumatano. Hata hivyo uamuzi rasmi kuhusu hilo bado haujafanyika, shirika la habari la dpa limeripoti.

Mawaziri hao wanatarajiwa kufanya tena mkutano kesho Ijumaa ili kutoa maelezo zaidi ikiwemo kuamua ni nani anayestahili kulipia vipimo hivyo vya lazima.

Hadi sasa, wasafiri wanaoingia Ujerumani kutoka nchi zinazotajwa kuwa zimeathirika zaidi na janga la Corona wanalazimika kukaa karantini kwa muda wa siku 14, japo utekelezaji wa hilo limekuwa vigumu. Kwa mujibu wa taasisi ya afya ya Robert Koch, mataifa mengi ya kigeni yanatajwa kuwa hatari.

Hata hivyo, kwa mujibu wa sheria hizo mpya watu wanaoingia Ujerumani kutoka Ufaransa, Uhispania, Ugiriki na nchi nyingi za Umoja wa Ulaya zinazotajwa kuwa na hatari ndogo, hawatalazimika kufanyiwa vipimo hivyo.

Maambukizi ya Corona yapindukia milioni nne Amerika ya Kusini

Brasilien Corona-Pandemie | Brasilianerin hält Gesichtsmaske mit Bolsonaro-Abbild in die Kamera
Raia wa Brazil akivaa barakoaPicha: DW/T. Milz

Kwengineko, idadi ya maambukizi ya virusi vya Corona katika mataifa ya Brazil na Argentina imepindukia milioni 4. Takwimu hizo zikionyesha wazi jinsi mataifa hayo ya Amerika ya Kusini yanavyolemewa na janga hilo.

Wazizi wa afya wa Peru Pilar Mazzeti amesema: "Wamechunguza hizi takwimu tangu mwanzoni mwa mwezi Machi, mwanzoni kabisa mwa janga la virusi vya Corona na hadi wiki ya mwisho ya mwezi Juni, wamebaini kwamba kuna takriban visa elfu 20 vya maambukizi ya Corona."

Brazil imerekodi maambukizi 67,860 huku watu 1,284 wakifariki kutokana na ugonjwa huo wa Covid-19 jana Jumatano. Hii inafikisha idadi jumla ya maambukizi nchini humo kuwa 2,227,514 na vifo 82,771.

Rais wa Brazil anayeegemea siasa za mrengo wa kulia Jair Bolsonaro amekuwa akipuuza uzito wa janga hilo la Covid-19. Bolsonaro amekutikana na virusi hivyo baada ya kufanyiwa vipimo jana Jumatano, hatua ambayo huenda ikavuruga mipango ya ziara yake aliyokuwa aifanye Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo wiki hii.

Na katika nchi jirani ya Argentina, idadi ya maambukizi imefika 141,900 huku nayo Peru ambayo ni ya pili baada ya Brazil kwa idadi kubwa ya maambukizi, imerekodi kiasi ya vifo 17,500 hadi kufikia sasa.

 

Chanzo: Reuters/dpa